WAGADUGU, BURKINA FASO

WAZIRI wa mambo ya nje wa Burkina Faso Alpha Barry,  ametangaza kwamba jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, imeamua kuisimamisha Guinea kwenye uanachama wake  kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini humo, ikiomba kurejeshwe uongozi wa katiba.

ECOWAS iliamua pia kutuma ujumbe wa kidiplomasia nchini humo ili kufanya majadiliano na viongozi wapya.

Viongozi wa nchi 15 wanachama wa ECOWAS walifanya mkutano wa dharura kwa njia ya mtandao kujadili mzozo wa Guinea.

Baada ya mkutano huo, waziri wa Burkina Faso wa mambo ya nje Alpha Barry, ambaye alishiriki kwenye mkutano huo, alisema ECOWAS iliamua kuisimamisha Guinea kwenye mamlaka zake zote za maamuzi.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, kwenye mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadogou, Barry aliongeza kuwa ECOWAS itaomba Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa kuidhinisha uamuzi wake.

Barry alisema, jumuia hiyo pia imeomba jeshi la Guinea kumuachilia huru Conde, na kuanzisha mchakato ambao utaruhusu kurejea kwa uongozi wa kikatiba.Ujumbe wa upatanishi wa ECOWAS unatarajiwa kuwasili Guinea.