CONAKRY, GUINEA

WAKUU wa mataifa ya Afrika Magharibi wamewawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi nchini Guinea na kutoa wito wa kufanyika uchaguzi katika kipindi cha miezi sita, ili kurejesha haraka utawala wa kiraia,baada ya wanajeshi kumpindua rais Alpha Conde mwezi huu.

Jumuiya ya kiuchumi ya kanda hiyo, ECOWAS, yenye mataifa 15 wanachama, tayari iliisimamisha Guinea baada ya mapinduzi hayo ya Septemba 5, yaliyoongozwa na kamanda wa vikosi maalumu, aliyemteka rais na kutangaza kipindi cha mpito wa kisiasa.

Uasi wa kijeshi nchini Guinea ulichochea wasiwasi wa kimataifa kuhusiana na kuporomoka kwa demokrasia katika kanda ya Afrika Magharibi, na kutoa ulinganisho na Mali, ambayo ilikumbwa na mapinduzi tangu Agosti mwaka jana.

Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Jean Claude Kassi Brou, alisema kwamba wakuu hao wa mataifa walisisitiza kuwa kipindi cha mpito laazima kiwe kifupi sana, baada ya mkutano wao mjini Accra, Ghana, kujadili mzozo wa Guinea.