ZASPOTI
MKURUGENZI wa ufundi wa Arsenal, Edu, ametetea sera ya uhamisho ya washika bunduki hao huku klabu ikiwa mkiani mwa Ligi Kuu ya England baada ya vipigo vitatu mfululizo.
Arsenal ilitumia zaidi ya pauni milioni 150 kwa usajili mpya msimu huu wa joto, zaidi ya klabu yoyote ya ligi hiyo.
Lakini kikosi cha Mikel Arteta kimeanza msimu wa ligi kwa kufungwa na Brentford, Chelsea na Manchester City.
“Nadhani lazima tuone muktadha mpana kuliko fedha tu,” Edu aliiambia Sky Sports.
“Tulisajili wachezaji sita walio chini ya umri wa miaka 23, ambao unamaanisha mengi kulingana na mipango yetu.
“Tulianza kupanga kikosi hichi mwaka mmoja uliopita kwa suala la kuimarisha timu na kujaribu kupata msingi bora. Tunapaswa kusawazisha kikosi vizuri.”
Mlinzi wa England, Ben White alikuwa usajili wa bei ghali zaidi wa washika bunduki, akijiunga kutoka Brighton kwa pauni milioni 50.
Pia walimsaini Albert Sambi Lokonga, Martin Odegaard, Aaron Ramsdale, Nuno Tavares na Takehiro Tomiyasu.
Arsenal haipo kwenye michuano ya Ulaya msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 1995, na wameanza vibaya kampeni ya ligi kwa miaka 67.
“Tunahitaji kikosi kuwa katika nafasi nzuri mwishoni mwa msimu kwa sababu sio tu ya ‘XI’ ya kwanza”, alisema Edu, mchezaji wa zamani wa Arsenal.
“Tunahitaji msingi na tunahitaji mafanikio.
“Ambapo tulihitaji kutumia fedha kubwa ilikuwa katika nafasi ya beki wa kati. Hapa ndiyo mahali ambapo tulihitaji mtu aje hapa na mara moja awe na athari kwa timu ya kwanza iliyo na wasifu sahihi kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Huyo alikuwa Ben White. ”
Edu, alisema, inaumiza kuiona Arsenal ikiwa chini ya msimamo, na bado haijafunga bao kwenye ligi msimu huu.
“Sitaki kuiona klabu hapo, lakini, nataka kuiona timu ikicheza pamoja,” alisema.
“Ninaelewa hali ni ngumu sana, lakini, wacha tuhukumu timu wakati wanacheza pamoja.”
Mbrazil huyo, ambaye aliteuliwa mnamo Julai 2019, alisema alikuwa, mwenye furaha na biashara ya majira ya joto.
“Huu ndio mpango ambao tulianza kutekeleza mwaka mmoja uliopita”. alisema.
“Mipango yote, hatua zote, michakato yote ambayo tuliweka pamoja, tulitekeleza”.(BBC Sports)