NA LAYLAT KHALFAN

KIKOSI cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU), kimesema kutolewa kwa elimu ya kujikinga na majanga mbali mbali ya moto itawezesha jamii kuchukua tahadhari pindi yanapotekea majanga hayo.

Ofisa Mkaguzi wa Kikosi hicho, Haji Khatib Hassan, aliyasema hayo wakati akiwapatia mafunzo ya kujikinga na majanga ya moto na utumiaji wa vifaa vya kuzimia moto kwa wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar, Maruhubi.

Alisema ili jamii ijikinge na majanga hayo, kikosi hicho kinachukua jitihada za makusudi kwa kupita kila taasisi kwa ajili kutoa elimu sahihi ya kujiepusha na majanga kama hayo.

Alisema mafunzo hayo ni moja kati ya majukumu ya kikosi hicho na ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa taasisi za serikali, binafsi na wananchi kwa ujumla.

“Ndani ya jamii zetu mara nyingi kunatokea majanga ya moto na kuathiri mali na watu hivyo tukitoa elimu hii mara kwa mara katika maeneo tofauti itasaidia kupunguza athari kubwa zinazotokezea,”alisema.

Ofisa Uhusiano wa bohari hiyo, Haji Omar, alisema kufuatia mafunzo hayo, wafanyakazi watakuwa tayari kupambana na majanga ya moto yatakapotekea kwa hatua za awali iloi kudhibiti madhara.

Omar alisema kutokana na kuwepo kwa majanga hayo ndani ya jamii, kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia mafunzo hayo ili yanapotekezea waweze kuyakabili  kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo, walisema wamenufaika na elimu waliyopatiwa kwani wameweza kufahamu aina mbali mbali za moto na jinsi ya kupambana nao pale unapotokea.

Sambamba na hayo waliahidi kuitumia taaluma waliyopatiwa kwani itawasaidia katika kuyakabili majanga yatakapotokezea huku wakikitaka kikosi hicho kuendelea na elimu katika taasisi mbalimbali.