YAOUNDE, Cameroun
NYOTA wa soka wa zamani wa Cameroun, Samuel Eto’o, atangaza kugombea urais wa Shirikisho la Soka la Cameroun (FECAFOOT). Tangazo hilo lilitolewa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Nimeamua kuchukua uamuzi huu kwa sababu ya kuipenda Cameroun na kupenda soka yetu”, alieleza, Eto’o katika taarifa yake.
Aliandika pia, “Ni wakati wa kujenga upya mpira wetu”. Baada ya uvumi kadhaa, Eto’o ameamua kuwa mgombea wakati kuna utata juu ya marufuku ya uraia mara mbili nchini Cameroun.

Eto’o alikuwa na uraia wa Hispania wakati alipokuwa huko.Miongoni mwa masharti yanayotakiwa kuwa mgombea wa urais wa FECAFOOT ni marufuku ya kuwa na utaifa wa kigeni.

Eto’o atakuwa kigogo wa tatu wa zamani kugombea urais wa shirikisho hilo.
Hata hivyo, bado haijulikani ikiwa ugombea wake utathibitishwa ambapo uchaguzi umepangwa kufanyika Disemba 11.