NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)

UGONJWA a kifua kikuu (TB) ni maambukizi yanayosababishwa na vimelea  (mycobacterium tuberculosis) ndani ya mapafu ya mwanaadamu

Ugonjwa wa TB ni aina ya ugonjwa ambao mtu huwa na viini vingi vya TB vinavyoishi mwilini mwa binaadamu na hivyo kumsababishia madhara.

Kwa kawaida mtu hujihisi mgonjwa, na mara nyingi huambukiza wengine viini vya TB. Ugonjwa wa TB unaweza kuwa sehemu yoyote mwilini mwa binaadamu lakini huathiri mapafu. Dalili za kawaida za ugonjwa wa TB ni kukohoa, homa, kukosa hamu ya chakula, kukonda, unyonge, kutoka jasho usiku na kuchoka.

Katika makala haya tunazungumzia namna ya kinga ya kifua kikuu dhidi ya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano.

Hivi karibuni baadhi ya wataalamu wa afya walikutana Zanzibar na kujadili namna ya kuwakinga watoto dhidi ya kifua kikuu baada ya kuonekana kuweko kwa tatizo hasa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kutokana na ripoti ya utafiti wa mwaka 2020 iliotolewa na  Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kupitia Programu Shirikishi UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma, imeonekana kwamba ni watoto 4 kwa kila watoto 10 (40%) wanaoishi na wagonjwa wa Kifua Kikuu cha Mapafu wamepatiwa dawa kinga ya Kifua Kikuu (IPT).

Kutokana na ongezeko hilo, inaonesha kwamba huduma hii ya dawa kinga kwa watoto haijatumika ipasavyo katika jamii yetu.

Hivyo, wizara imewashauri wazazi na walezi kuhamasika kuitumia huduma hii kwa ajili ya kukinga maambukizi ya Kifua Kikuu kwa watoto.

DAWA YA KINGA YA TB KWA WATOTO

Dawa kinga ya Kifua Kikuu (IPT) ni dawa wanayopewa watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa ajili ya kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, iwapo ndani ya nyumba kuna mgonjwa wa Kifua Kikuu cha ndani ya Mapafu.

Dawa hii hupewa watoto wenye umri chini ya wa miaka 5 ambao wazazi, jamaa au walezi wanaugua ugonjwa wa Kifua Kikuu

Watoto wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kuanzia umri wa miezi 12 hadi miaka 5

Kwa mujibu wa wataalamu dawa hizi hutolewa  kwa watoto kwa muda wa kipindi cha miezi sita mfululizo ambapo kila siku hutakiwa kumeza mara moja tua katika kipindi hicho cha miezi sita.

Hata hivyo wataalamu hao walisema kuwa hata kama mtoto hatakuwa na dalili yoyote ya kifua kikuu atalazimika kumeza kwa kuwa anakuwa katika hatari ya kupata maambukizi kutokana na kuishi na wagonjwa wa TB.

Kwa wale watoto ambao wanaonyonya hutakiwa kufanyiwa uchunguzi kwa kupima makohozi na X – ray.

Faida kubwa inayopatikana ni pamoja na kuzuia kupata Kifua Kikuu kwa watoto wenye chini ya umri wa miaka 5, kupunguza maambukizi katika jamii.

WATAALAM WANASEMAJE?

Akizungumza na makala haya Sabrina Kassim Ali Daktari kutoka kiliniki ya ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja alisema mbali na muitikio wa wagonjwa na wahudumiaji kuwa mkubwa lakini kuna changamoto nyingi zinazorejesha nyuma tiba hiyo kwa watoto dhidi ya kinga ya TB.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto kwa ajili ya uchunguzi na badala yake kusikiliza maneno yasiyo na ukweli.

“Wakiona watoto hawana dalili ya kifua kikuu hawafuatilia uchunguzi wala matibabu yoyote jambo ambalo lina sababisha na wao kuugua ingawa kwa baadae”, alisema.

Daktari Sabrina aliwanasihi wanajamii kufuata taratibu za kinga hasa kwa wale familia ambayo yenye mgonjwa wa kifua kikuu kwa kuwapeleka watu wote wanaoishi nao kwa ajili ya uchunguzi.

Nae Maryam Juma Suleiman wa Kibweni, mama mwenye mtoto alieguwa  kifua kikuu kwa  muda wa miaka 3 sasa na ambae ana umri wa miaka 7 alisema  alimbaini mtoto wake na ugojnwa baada ya kuhangaika sana.

“Nilienda mpaka kwa waganga wa jadi kutafuta matibabu ya mtoto wangu lakini siku moja baada ya kutulia na kufikiri sana nilipata mtu na kunishauri kucheki  kifua kikuu”, alisema.

Alifahamisha kuwa mara baada ya kufika hospitali kuu ya Mnazi mmoja mtoto wake alibainika na ugonjwa wa kifua kikuu.

Maryam alisema iko haia ya Kuanzisha matibabu wagonjwa wenye kifua kikuu kwa kushirikiana na wahudumu wanaojitolea katika jammii ili kupunguza changamoto zinazoweza kutokea katika jamii.

DALILI ZA KIFUA KIKUU

Kikohozi cha muda wa wiki mbili au zaidi, Kupata makohozi ambayo yamechanganyika na damu hata kama ni moja, homa za hasa wakati wa jioni

Dalili nyengine ni Kutokwa na jasho jingi ambalo si la kawaida wakati usiku, Kukonda au kupungua uzito wa mwili.

Jamii inapaswa kuwahi mapema katika vituo vya afya pindi tu waonapo dalili yoyote ile katika hizo nilizozibainisha.

UHUSIANO WA KIFUA KIKUU NA UKIMWI

Ni dhahiri kwamba upo uhusiano kati ya ugonjwa wa kifua kikuu na maambikizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Kwa kawaida dalili za Kifua kikuu hujidhihirisha mara tu kinga ya mwili  inapopungua na kushindwa kukabiliana na uambukizi wa vimelea vya Kifua kikuu.

Hali hii husababisha maradhi  ya kifua kikuu kuwa maradhi nyemelezi yanayojitokeza mwanzo na kusababisha vifo  kwa watu wanaoishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI (VVU).

Hata hivyo, haimaanishi kwamba kila mwenye Kifua kikuu ana UKIMWI. Au kila anayeishi na maambukizi yanayosababisha virusi vya UKIMWI ana Kifua kikuu.

Hapa Zanzibar maambukizi ya VVU baina ya watu wanaogundulika na Kifua kikuu ni wastani wa asilimia 15 hadi 20 kila mwaka.

MATUMAINI YA KUPAMBANA NA KIFUA KIKUU ZANZIBAR

Jambo la kutia matumaini ni kwamba hata kama mtu akigundulika na magonjwa yote mawili Kifua kikuu na VVU (UKIMWI) zipo dawa za  kutibu Kifua kikuu na dawa za  kupunguza makali ya VVU ambazo hutolewa bila ya malipo na kuimarisha afya ya mgonjwa.

Kwa mujibu wa Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na. Watoto,ya mwaka 2021-22 ilisema kuwa serikali itatoa huduma za matibabu ya Kifua kikuu ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwenye vituo vyote Mijini na mashamba ambapo katika kituo chochote cha afya au hospitali za Serikali, baadhi ya vituo na hospitali za watu binafsi huduma za uchunguzi na matibabu ya Kifua kikuu hutolewa bure bila ya malipo yoyote.

Aidha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kutokomeza maradhi haya, ikiwa ni pamoja na kununua mashine nne (4) za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya Kifua kikuu kwa njia ya vinasaba (Gene Xpert machine).

Sambamba na hilo wizara inaendelea kutoa elimu ya Afya pamoja ya namna ya   kujikinga  na maradhi haya sehemu mbali mbali zikiwemo maskuli,  pamoja na sehemu nyengine mijini na vijijini pindi tu mgonjwa anapogundulika.

Sambamba na hilo, lakini Wizara ya afya kupitia Program ya Kifua kikuu imekuwa ikiwatembelea majumbani, wagonjwa wote wenye vimelea na kuwachunguza watu wote waliokaribu na mgonjwa ili kuwagundua mapema.

Ushirikishwaji wa kila mdau ni muhimu katika kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo la kifua kikuu Zanzibar.

CHANGAMOTO YA KUPAMBANA NA UGONJWA WA KIFUA KIKUU ZANZIBAR

Ili kutokomeza ugonjwa huu hapa Zanzibar kila mmoja ana wajibu wa kupambana na ugonjwa huo na sio jukumu la Wizara ya afya pekee, bali jamii yote inatakiwa kuhusika ikiwa ni pamoja na viongozi mbalimbali katika ngazi zote iwe za kisiasa na za kijamii kama Wabunge, Wawakilishi, Mameya, Madiwani, Masheha, viongozi wa Dini na viongozi wengine wote wa jamii.

Inaonesha kuwa licha ya jitihada zinazochukuliwa, bado kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Kifua kikuu ambao hawajatitokeza na kupata tiba sahihi, na hivyo kuendeleza maambukizi katika jamii. Ili kutokomeza kabisa maradhi haya ni lazima tuwagundue na kuwatibu wale wote ambao wana ugonjwa huu.

Pamoja na msisitizo huo, Wizara ya afya inawakumbusha wananchi wote kwamba mnao wajibu wa kufika katika vituo vya afya mara tu mtu yoyote anapoonyesha dalili za maradhi haya ambazo naomba nizitaje kama ifuatavyo:-

Kuwahi mapema hospitali na kupatiwa tiba sahihi mapema ndiyo njia kubwa katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu kuenea katika jamii.

Ni haki ya mgonjwa kumuomba daktari ampime makohozi hasa akiwa amejigundua anakohoa kwa muda mrefu bila nafuu ya dawa anazopewa hasa kwa kuwa kuna baadhi ya wagonjwa wamekuwa hawatumii dawa ipasavyo.

WITO KWA JAMII

Ni wajibu kwa jamii kwa ujumla, taasisi mbali mbali katika jamii, viongozi wa ngazi mbali mbali, viongozi wa dini, na vyombo vya habari Kulifahamu tatizo la kifua kikuu’ na kushirikiana na Wizara ya afya kupitia Programu shirikishi cha UKIMWI, Homa Ya Ini, Kifua kikuu na Ukoma, kuwafikia na kuwaibua wale wote wanye maradhi haya.

Aidha ipo haja kwa Viongozi wa ngazi zote iwe kiserikali, kisiasa na kijamii kuzungumzia Kifua kikuu kwenye vikao vyetu na mikutano ya hadhara na kadhalika ili kufanikisha azma ya kupunguza maambukizi ya Kifua kikuu na kushajihisha wale wote wenye dalili za maradhi haya kufika mapema hospitali na vituo vya afya  kwa ajili ya uchunguzi na  tiba sahihi ya Kifua kikuu.

Pia kuzingatia elimu ya afya pamoja na maelekezo mbali mbali yanayotolewa na wataalam wa afya katika sehemu mbali mbali katika kudhibiti ugonjwa huu wa Kifua kikuu.

Ili kuweza kuutokemeza ugonjwa huo hapa nchini ipo haja ya jamii kukumbuka ule usemi usemao ‘Kinga ni bora na rahisi kuliko Tiba’