Hutumia kipimo cha-‘Bobay’  ili kuwa na madini joto

 NA HAJI NASSOR, PEMBA

“MAJI ya chumvi yakitoka baharini, huwa na joto la sifuri au kisaynasi inaitwa ‘zero Bobay’, hapo sasa lazima kuyaingiza kwenye bwawa ‘reserve’ ili kuyavumbika,’’

Ndivyo alivyoanza mtaalamu na mkulima wa bidhaa ya chumvi ya mawe, Bakari Shaaban Bakari aliyeko bahari ya mjini Kiungoni Wete Pemba, wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya.

CHUMVI NI NINI?

Chumvi kwa maana ya kemia ni kampaundi inayofanywa na ‘ion’ yaani  anioni  yenye chaji hasi na ‘Calcium  yenye chaji chanya baada ya bezi kuunganika na aside au metali yoyote.

Hata hivyo, kuna aina nyingi za chumvi kutokana na elementi mbalimbali na hizi kwa jumla haziwezi kuliwa na bindamu, kwa mfano chumvi ya aside, chumvi ya muungano.

Kwa bahati mbaya, chumvi inayotumiwa na watu wengi haina madini ya kutosha ya sodium na chloride kutokana na kutengenezwa upya viwandani kwa kusafishwa (refined).

Utumiaji wa chumvi sahihi na kwa kiwango kinachotakiwa, una faida nyingi mwilini, ikiwemo kuimarisha na kudhibiti shinikizo la damu, kuboresha ufanisi wa misuli ya mwili, kuboresha ufanisi wa ubongo.

Kwani, ubongo wa binadamu pamoja na uti wa mgongo, vimo katika mfumo wa maji chumvi uitwao ‘cerebrospinal fluid).

BOBAY NI NINI?

Ni nambari za kawaida zinazotumika kuangalii ujoto wa maji ya chumvi, yanapotolewa baharini hasa kwa ajili ya kuyatayarisha kwa uzalishaji wa chumvi ya mawe.

Namba hizo, zimo kwenye kifaa kirefu cha kigae kinchoitwa hydrogen.

Kwenye kifaa hicho, zimo nambari zilizo anzaia zero hadi 30, ambapo unapokiweka kwenye maji ya bahari yaliotengwa bila ya kuingilia na mengine, hupanda kulingana na ujoto wa maji husika.

KWANINI KITUMIKE KWENYE UZALISHAJI WA CHUMVI?

Kisayansi mtaalamu huyo mzaliwa wa Kenya, anasema maji ya bahari yote duniani, huwa na ujoto ‘0’ ambapo hilo huwezi kulijua kwa kuangalia kwa macho pekee, wala kuingiza mkono, bali lazima utumie Hydrogen na kuangalia Bobay zilivyopanda ama kushuka.

“Ukiingiza tu kifaa cha hydrogen, basi utaona namba zinapanda, kuanzia sifri hadi 30, itategemea na ujoto wa maji yalivyo,’’anasema.

HATUA ZA UZALISHAJI WA CHUMVI YA MAWE KISAYANSI

Akizungumza na makala haya mkulima huyo wa chumvi anasema kuwa hatua ya kwanza ni kujenga bwawa ‘Reserve’ lililokaribu na bahari, na kisha ni kuingiza maji ya bahari.

Bakari alisema baada ya hapo bwawa lake lina upana wa mita 12, wastani wa pima 6 za za mkono na urefu wa mita 24 sawa na pima 12 za mtu mzima.

“Bwawa hilo moja hubeba lita 600 ya maji kutoka baharini, na kisha kwenye uvunaji hujipatia kati vipolo 80 vyenye ujazo wa kilo 50, sawa na 4,000, alisema.

Anazidi kufafanuwa kuwa, maji ya chumvi asili yake yana chumvi aina zaidi ya 200, ikiwa ni pamoja na Magnesium, sodium corbinate, ambayo inayotumika na binaadamu ni chumvi aina ya sodium chloride.

“Kisha hapo maji yatakaa kwa muda wa siku tatu hadi nne na lazima uwe na bwawa jengine, ambalo kisayansi linaitwa ‘condenser’.

“Maji ya chumvi ukiyaweka kwenye bwawa la kwanza ‘reserve’ kisha yanaweza kupanda ujoto ‘Bobay’ hadi kufikia kati ya tatu hadi nne,’’anasema.

Aliongeza kuwa baada ya hatua hiyomaji yaliyomo huhamishwa kwa kutumia mpira wa maji, na kiyaingiza kwenye bwawa jengine.

“Wakati unayingiza kwenye bwawa hilo, tayari joto la maji hayo kutoka baharini, yatakuwa limeshapanda, na sasa utalazimika kuyagawa wenye mabwa mawili tofauti.

Hivyo sasa maji yatalazimika kuwekwa kwenye condenser nambari moja na condenser nambari mbili, ambapo baada ya siku tano sasa ‘Bobay’ hupanda hadi kufikia kati ya 10 hadi 15”, alisema.

KWANINI MAJI YAPADE JOTO JUU ‘Bobay’?

Alifahamisha kuwa Kisayansi, maji ya bahari unapoyachukua na kuyahifadhi sehemu bila ya kuingiliwa maji mengine kama ya mvua, huzalisha joto kali mno, ambapo baadae hukauka na kufanyika kitu mithili ya chumvi.

“Wakati wa hayo yameshafika ndani ya Condenser nambari 2, yakiwa na ‘Bobay’ 10 hadi 15, huendelea kuvumbikwa hapo kwa siku 4, na yatakuwa yanapimwa kila siku, na hadi yatakapofikia ‘Bobay’ 20 kisha huhamishwa tena.

Mtaalamu huyo, anabainisha kuwa, sasa hapo maji hayo yatakuwa mazito mithili yamafuta ya nazi, na yatahamishwa tena kwenda kwenye bwawa nambari 3, condenser number three”.

Wakati yakifika ndani ya bwawa hili nambari tatu, yakiwa na ujoto wa uniti 20, yataachwa hapo, hadi lipande tena na kufikia‘Bobay’ au uniti 25 huhamishwa na kusafirishwa hadi kwenye bwawa nambari nne, kitaalamu linaloitwa Evaporator or crostalyser”, anaongeza.

Anasema dalili za kuelekea kuzaliwa kwa chumvi, ni kuona kwenye bwawa, kuwepo kwa ukungu ukungu au utandu utandu ambao huo ndio chanzo cha chumvi husika.

“Juu ya maji ukiona kama kuna vumbi vumbi au ukungu fulani, basi hiyo na chumvi inaanza kushikana na kisha kadiri unavyokuwa mzito, huanguka chini,’’anaeleza.

Kwa kwaida chumvi huanza kuzaliwa juu ya maji, ambapo kisha huanguka chini ndani ya ‘bwawa’ na kisha kadiri ‘Bobay’ zinavyopanda, na chenga  chenga huongezeka,’’anafafanua.

Ndani ya bwawa hilo namabri nne, mtaalamu na mkulima huyo anafafanua kuwa, ukiona sasa kipimo chako cha hydrogen kinaonesha Bobay’ zimeshafikia 26 hadi 27, hapo chumvi sasa imeanza kuzaliwa.

“Hapo sasa hata kwa macho ya kwaida, unaweza kuanza kuona chenga chenga za chumvi, ambapo sasa husubiriwa kupevuka kwa siku 10 tu, kabla ya kuanza kuvunwa,’’anaeleza.

Tokea siku ya kwanza ya kuyahifadhi haji hadi kufikia siku ya kuvunwa chumvi, kwa kilimo cha siku ya kwanza, huwa ni kati ya siku 27 hadi 30.

UVUNAJI WA CHUMVI

Akizungumzia hatua ya uvunaji, mkulima Bakari, alisema kwanza, chumvi ili ipatikane hakuna haja ya bwawa nambari nne, likauke kama wengine wanavyofikiria.

Bali hatua zilizoelezwa hapo, ni sawa na uvumbikaji wa maji ya bahari, kwamba chumvi hii ya mawe, unaweza kuvuna na bwawa likiwa na maji yake.

“Kwani mkulima huyo na mtaalamu wa uzalishaji chumvi, anasema, kwanza unatumia majiti maalum yaliotengenezwa mithili ywa mfano ‘mop’ au ‘rake’.

“Hili huwa inakusanyiwa, maana haishauriwi kutumia mikono, kwa vile inaweza kuua alama za kiganja, na kupoteza alama za finger print, anafafanua.

Anasema, unaikusanya pamoja vishungu vishungu na kufanya kuoikosha kwa maji hayo hayo ya chumvi, na baada ya dakika 5 hadi 10, unanza kuingiza kwenye chombo.

KWANINI CHUMVI ITIWE MADINI JOTO?

Madini joto ni aina ya unga unga fulani, ambao kazi yake kubwa ndani ya mwili wa mwadamu, ni pamoja na kukazanisha mifupa.

Vyakula karibu vyote vinavyotoka baharini, hujengwa na madini joto, iwe samaki au chaza.

“Sasa ili wananchi wapate madini hayo muhimu, ndio maana huwekewa kwenye chumvi, na kwa mfano sayansi inataka kuwa madini joto yenye ujazo wa kijiko kimoja cha kulia, iyayushwe kwa maji lita 10.

“Hivyo kwanza uwe na maji yenye ujazo wa lita 10, unachanganya pamoja na madini joto, ujazo wa kijiko kimoja cha chai, na kisha unaimiminia chumvi na kichanganya pamoja,” anaeleza.

Madini joto yanafaida kubwa mwilini wa binadamu, ikiwa ni pamoja na, kwa mama mjamzito kupata kizazi bora.

Kinga dhidi ya maradhi ya kuvimba shingi ‘goiter’ kupata ukuaji mzuri wa watoto, kujenga ubongo, kutozaa watoto weye ulemavu wa akili.

WATEJA WA CHUMVI WANASEMAJE?

Mfanyabiashara Khamis Muhidi Khamis wa Chake Chake, anasema chumvi hiyo ndio pekee, anayopenda kutokana na kuzalishwa kitaalamu.

Anasema, kwanza ni nyeupe, imeingizwa madini joto na ukali wake hausababishi uchungu kama zilivyo chumvi nyingine.

Nae Omar Haji Makame wa Wete, anasema kwa miaka minne sasa, ameachana na kuagizishia bidhaa hiyo kutoka Mkoani Tanga na Mbombasa Kenya, bali ananunua kwa mkulima huyo.

Mwanaisha Hamad Hassan wa Mchanga mdogo, anasema yeye na wenzake wamekuwa wakitumia chumvi hiyo wanayogaiwa wanapokwenda siku za mavuno.

COSTECH

Mwezi Disemba mwaka jana, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknologia ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘COSTECH’ kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar, iliendesha mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari na watafiti.

Moja ya malengo ya mafunzo hayo, ni kuwaleta karibu waandishi na watafiti, ili kufanya kazi kwa karibu na kuwasaidia wabunifu, ili kupata taarifa za kitafiti.

Ndio maana wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Mdhamini wa Tume ya Mipango Zanzibar kisiwani Pemba Dadi Faki Dadi, alisema tafiti zinaumuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

Alisema tatfiti zilizofanywa na kisha kuishia kwenye makabati, haziwasaidii wananchi, hivyo ni wajibu wa watafiti hao, kukutana na waandishi wa habari, ili kuwawasilishia wananchi na watunga sera.

Kwenye mafunzo hayo, Kaibu Mkurugenzi wa Utawala na Maarifa kutoka ‘COSTECH’ Dk. Bunini Manyilizu, alisema utafiti na sayansi ndio kila kitu, ikiwa taifa linataka kusonga mbele.

“Ni kweli zipo tafiti kadhaa zilizofanywa na watafiti, lakini kwa vile kuna mpasuko wa kutowasiliana na vyombo vya habari, hazisaidii, ndio maana ‘COSTECH’ ikandaa mafunzo haya,’’anasema.

Hivyo, anasema sasa anatarajia waandishi wa habari watawaibua watafiti, wabunifu, wanasayansi ili kutangaaza kazi zao.