Ni binti mwenye uoni hafifu mwenye shahada ya uhasibu
NA MWANDISHI WETU
“NILIZALIWA nikiwa sioni kabisa, lakini miaka mitatu baadae nilifanyiwa operesheni, nikiwa na uoni hafifu hadi nikamaliza dara sa 12,’’ndio maneno ya mwanzo ya Faiza Said Kassim.
Mwaka 2019 Faiza alikuwa mmoja kati ya wahitimu wa elimu ya digrii kwa fani ya uhasibu, kwenye Chuo cha Usimamizi wa Fedha Chwaka Zanzibar.
Mama wa Faiza, Bi Habiba Yussufu Alawi anasema kati ya mimba zake tano, ya Faiza ndio ambayo ilimtia mashaka na kulazimika kuhudhuria hospitali kila muda.
Baada ya kumzaa, aligundua hana uoni kamili, ingawa mwaka mmoja na nusu badaae, alimikimbiza hospitali kwa uchunguzi na alipotiza miaka mitatu alifanyiwa upasuaji.
“Faiza alifanyiwa operesheni hospitali ya Muhimbili, na baada ya kukua na kuanza elimu ya msingi alianza kutumia miwani maalum,’’anasema.
Mwenyewe anasema, alikuwa na uoni hafifu tokea kupata kwake fahamu, na alianza darasa la kwanza skuli ya msingi ya Michakaini Chake chake akiwa kwenye elimu mjumuisho.
“Ijapokuwa sio lile darasa rasmi, lakini na mimi nilichanganywa na wengine wenye uoni kamili, na kuanzia hapo ikawa mimi na miwani ni ndugu,’’anasimulia.
Aliendelea na msomo yake ya msingi skulini hapo, akijinasibu kuwa tokea elimu yake msingi hadi anamaliza digrii yake ya uhasibu mwaka 2019, hakuwahi kufeli wala kurejea mitihani.
“Mimi ilikuwa nafasi yangu ya darasani kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la 12, ni kati ya tatu hadi tano, na hata nilipokuwa chuo sikuwahi kupata mitihani ya marejeo,’’anaeleza.
Akiwa skuli ya msingi ya Michakaini, anasema alikuwa na ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzake, na wala hakuwahi kubaguliwa kwa sababu ya uoni wake hafifu, wala miwani aliyokuwa akiivaa.
Analolikumbuka kuanzia hapo hadi anasoma digrii chuo cha Fedha Chwaka, ilikuwa nafasi yake ni ya meza ya mbele, jambo ambalo hata wanafunzi wenzake walimzoea.
Mazingira ya skuli kwa wakati huo pamoja na kwamba kulikuwa na ushiriki wa michezo na mambo mengine mbali mbali, lakini ulemavu wake wa uoni hafifu haukuwa mzigo.
Pamoja na kwamba kwa baadhi ya siku alikuwa akiuumwa mno na kichwa au kuwashwa na macho kutokana na hali yake, lakini skuli hakuwa mtoro na alikuwa na hamu.
“Ingawa mama ni mkali kwenye mambo ya elimu, lakini na mimi pamoja na ulemnavu wangu wa uoni hafifu nilikuwa na juhudi za ziada na kisha nilipata matokeo mazuri,’’anabainisha.
Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, alifanikiwa kujiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya Connecting Continet iliyopo Mgogoni Chake chake.
Hapo hakuwa na kazi ngumu, iliyosababishwa na ulemavu bali anayakumbuka vyema mashirikiano na umoja aliyooneshwa na waalimu na wanafunzi wake.
“Nilikuwa natumia miwani yenye namba 10 (+10) ambayo ilikuwa mikubwa, na hivyo wanafunzi walinigundua kuwa nna ulemavu wa macho, lakini sikuwahi kupata unyanyasaji,’’anasema.
Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari skulini hapo, Faiza aliumwa sana na kichwa na wakati mwengine akielezea kuona vitu mithili ya viduara duara machoni mwake.
Akiwa anaendelea kutumia miwania yake yenye mamba ‘+10’ kichwa kilizidi kumuuma mno, na kupelekwa tena hospitali ya Chake chake ingwa tatizo lake lilishindikana na kuhamishiwa hospitali ya Mkoani Pemba.
Kesi ya maumivu yake, ililazimika kupelekwa hospitali ya ‘CCBRT’ Tanzania bara, na huko alielezwa kuwa jicho lake limeshaharibika mno na haliwezi kurejeshwa.
“Nilipofuka rasmi mwaka 2011, niliambiwa na madaktari na kuanzia hapo nikawa natumia jicho moja na sasa nimeshatimiza miaka 10 sasa nikiwa naendesha shuhguli zangu na jicho moja tu,’’alieleza.
Mama mzazi wa Faiza, anasema baada ya kuona hivyo, alikosa furaha na kukata tamaa ya mwanawe kuendelea na masomo ya ngazi ya chuo kutokana na kukosa jicho.
“Aliniambia anataka kuomba Chuo cha Fedha Chwaka Zanzibar, lakini mimi nilimkatalia kutokana na hali yake ya kuwa na jicho moja,’’alieleza mama yake.
Anasema, hakuwa tayari kumtafutia chuo mwanawe, kutokana na hali yake, ingawa baada ya Faiza kumkera mno, alimsaidia kuomba chuo na kufanikiwa kujiunga na ngazi ya cheti fani ya uhasibu mwaka 2012/2013.
“Ni kweli mama yangu baada ya kunishuhudia nikiwa na jicho moja, alikata tamaa, lakini nikamwambia mama akili zangu pamoja na jicho moja yako ‘fit’ kukosa jicho moja sio sababu,’’alieleza.
Faiza alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Fedha Chwaka kisiwani Unguja, kuanzia cheti na kumalizia digrii mwaka 2019 na hakuwahi kupata kurejea mitihani hata mara moja.
Anakumbuka vyema kuwa, kila mwaka wapo wanafunzi kati ya watatu hadi watano wamekuwa wakirejea nyumbani baada ya kufeli masomo kadhaa, ingawa yeye hakuwa miongoni mwao.
Kama kawaida anasema nafasi yake ya mbele ndio aliyokuwa nayo kwa muda mrefu, na alikuwa akimpata vyema mwalimu anaesomesha, na hakupata kikwazo chochote.
“Ukosefu wangu wa jicho moja, na hili jengine kuwa na uoni hafifu, haukunizia kuondoka Chuo cha Fedha Chwaka na dirii ya uhasibu, na sasa nipo mtaani,’’anasema.
Baada ya kumaliza masomo yake, alirejea kijijini kwao Vikunguni wilaya ya Chake chake Pemba, na sasa ameshatimiza miwili, akiisaka ajira kwa udi na uvumba.
“Nimeshafanya usaili zaidi ya mata tatu, na nimeshafanya maombi bil ya usaili mara tano, lakini hadi sasa ajira sijaiipata, ingawa husikia tunapewa kipaumbele wenye ulemavu,’’anasema.
Sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar nambari 9 ya mwaka 2006 kifungu cha 7 kinabainisha kuwa kwa mujibu wa masharti zinazohusiana na ajira na mafunzo ya amali.
Ambapo kimefafanua kuwa, hapana mtu atakayekataa kumuajiri mtu mwenye ulemavu mwenye sifa za kiwango cha chini za kuajiriwa.
Kifungu cha 8 (1) (b) kikfafanua kuwa, muajiri atatoa vifaa na kuvifanyia marekebisho pale itakapohitajika ka kumuwezesha mtu mwenye ulemavu kufanya kazi.
Nilipomuuliza Faiza ikiwa anadhani sheria yao inatekelezwa, alisema bado kuna kusua sua kwa waajiri, kutokana na kutowapa kipaumbele watu wenye ulemavu.
Hayo yakifanyika, lakini Azimio la ulimwengu la haki za watu wenye ulemavu Ibara ya 7, imezitaka nchi wanachama zilizoridhia mkataba huyo kufanya kazi kwa misingi ya usawa.
Ibara hiyo ikfafanua kuwa, usawa huyo hutakiwa baina ya watu wenye ulemavu na wasio kuwa nao, ili nao kumudu maisha yao kwa kufanya kazi walioichagua au kuikubali.
MAMA WA FAIZA
Habiba Yussuf Alawi, anasema mtoto wake huyo, ameshahangaika nae kumtafutia ajira hata ya tasisi binafsi, ingawa bado hajafanikiwa.
“Huwa tunaskiliza sana matangaazo ya nafasi ya kazi, na amekuwa akijitahidi kuomba na wakati mwengine anafanya usaili pekee mwenye ulemavu, lakini matokeo sio mazuri,’’anafafanua.
Anashauri kuwa, mwanawe na wengine ambao wameshahangaiko kusoma kwa shida, suala la ajira lisiwe la mashaka mashaka kwao.
Mratibu wa Idara ya watu wenye Ulemavu Pemba, Mashavu Juma Mabroku, akizungumza hivi karibu mjini Chake chake alisema kwa sasa kidogo kuna ahuweni kwa kundi hilo kuajiriwa.
“Ijapokuwa bado tatizo lipo, lakini wapo wenye ulemavu wanaona kwenye ofisi za umma, mfano wizara ya Elimu, wizara ya Habari, Afya lakini kundi kubwa na lenye sifa lipo nje,’’alieleza.
Waziri Wa Nchi Ofisi ya rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman akizungumza kwenye baraza la wawakilishi, alisema wizara haijawabagua watu wenye uleamvu.
Alisema, wamekuwa wakiajiriwa katika maeneo ambayo yanalingana na mazingira ya miili yao, ijapokuwa sasa wapo wengi wanaoajirika.
Waakati akiomba ridhaa, Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliahidi kuwapatia vijana ajira 30,000 katika sekta iliyorasmi na isiyorasmi ifikapo mwaka 2025.
Ingawa Dk. Mwinyi hakutaja idadi kwa kundi la watu wenye ulemavu watakuwa wangapi, lakini pia sheria yao imezingatia uwiyano huo.
MWENYE ULEMAVU ALIYEPATA AJIRA
Khamis Ali ambae anahuduma wizara ya elimu akiwa mwenye ulemavu wa ukosefu wa mguu mmoja, anasema baada ya kumaliza digrii alifanikiwa kupata ajira.
“Nilifanya usaili na wasio na ajira zaidi ya 20, wakati nafasi zilizokuwa zikitakiwa zilikuwa mbili, lakini yalipokuja majibu nilifanikiwa,’’anasema.
Anasema bado kundi la watu wenye ulemavu halijatazamwa ipasavyo ingawa waajiri wanasukumwa na sheria nambari 9 ya mwaka 2006.
Kijana Faiza ambae anadigrii ya uhasibu kwa miaka mitatu sasa, yuko kijijini kwao Vikunguni wilaya ya Chake chake akila, kulala na kuamka akiendelea kuomba ajira.