TEHRAN, IRAN

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA wamekipongeza kituo cha utafiti wa kilimo cha kutumia tekonolojia ya nyuklia cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria, imewanukuu wakurugenzi wakuu hao wa FAO na IAEA wakitoa pongezi hizo pembezoni mwa mkutano mkuu wa taasisi za kimataifa zinazojihusisha na usalama wa chakula na maendeleo endelevu duniani.

Rafael Mariano Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na Qu Dongyu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO wametoa pongenzi na shukrani kwa kituo hicho cha Iran cha uchunguzi wa kilimo unaotumia teknolojia ya nyuklia.

Pongezi hizo zilitokana na kazi kubwa na muhimu kiliyoifanya katika tafiti zake na kutumia njia bora za teknolojia ya nyuklia katika kilimo na uzalishaji mazao kwa manufaa ya wanadamu na viumbe wengine.

Kituo hicho kiko chini ya Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran.Mara kwa mara Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kwamba shughuli zake za nyuklia ni za amani na za kiraia kikamilifu ni kwa ajili ya manufaa ya wanadamu na viumbe wengine na wala Tehran haina mpango wa kumiliki silaha za nyuklia.

Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, ni haramu kumiliki silaha za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia, na ndio maana silaha za atomiki hazimo katika mikakati ya kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.