Yasema anafuata misingi ya demokrasia

NA KHAMISUU ABDALLAH

TAASISI ya Kijerumani ya kukuza na kuboresha demokrasia, utawala bora inayofanya kazi na asasi za kiraia, vyama vya siasa na wafanyakazi nchini (FES), imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kufuata misingi ya demokrasia nchini.

Akizungumza na Zanzibar Leo, ofisa miradi wa shirika hilo, Amon Petro kuhusu siku ya demokrasia ulimwenguni inayoadhimishwa Septemba 15 ya kila mwaka, alisema Dk. Mwinyi amepiga hatua kubwa ya kuendeleza demokrasia na utawala bora nchini.

Alisema katika moja ya jambo muhimu ambalo Dk. Mwinyi amelifanya kama kielelezo cha kuwashirikisha wananchi ni hatua yake ya kuunda mtandao wa SEMA na Rais ambao unawapa fursa ya kufikisha kero zao.

Aidha alisema hatua hiyo inakuza maendeleo nchini kwani inaonesha utayari was rais kushirikiana na wananchi moja kwa moja kwenye maeneo yao katika kuwatatulia changamoto zinazowakabili.

Alibainisha kuwa mfumo huo ni wa kupigiwa mfano kwani pia unaondosha woga na hofu kwa wananchi kujieleza mbele ya kiongozi wao wa nchi hali inayosaidia kutambua changamoto mbalimbali.

“Mfumo huu ni mzuri na adimu na mfumo wa kwanza barani Afrika wa kiongozi mkuu wa nchi kujitoa na kuwafikia wananchi moja kwa moja kusikiliza changamoto zao tunampongeza Rais Mwinyi”, alisema.

Mbali na hayo, alisema mfumo huo unaweza kuisadia serikali kupanga mipango yake ya maendeleo ikiwemo maji, barabara, afya na mambo mengine muhimu.

Alibainisha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anaendesha uongozi ambao unawapa uhuru wananchi kujielekeza hivyo aliwaomba wananchi kuitumia fursa hiyo.

“Kwa kweli viongozi wetu wametoa uhuru mkubwa sana kwa wananchi kwani hata katika chanjo ya korona viongozi wetu wametoa fursa kwa anaetaka kuchanja achanje na asiyetaka halazimishwi,” alibainisha.