CONAKRY, GUINEA

WAKUU wa kikosi maalum cha jeshi la Guinea kilichompindua rais Alpha Conde madarakani,wameahidi kuunda serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.

Kikosi hicho kinachoongozwa na kanali Mamady Doumbouya kilimkamata Rais Conde na kuwapiga marufuku mawaziri na viongozi wengine wakuu kusafiri nje ya nchi.

Doumbouya hakutoa maelezo kuhusu watakaojumuishwa kwenye serikali hiyo ya mpito.

Aidha hakutangaza tarehe ya kuandaa uchaguzi ili kurejesha utawala wa kidemokrasia.

Hayo yakijiri jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS ilisema itaandaa mkutano wa kilele kuhusu Guinea.

Hayo ni kulingana na waraka ambao shirika la Habari la Reuters limepata,hata hivyo msemaji wa ECOWAS hakuweza kutoa kauli ya moja kwa moja.

Mapinduzi hayo yalilaaniwa vikali na mataifa pamoja na mashirika ya kimataifa yakitia shinikizo kutaka Rais Conde aachiliwe huru.