CONAKRY,GUINEA

WAKUU wa kikosi maalumu cha kijeshi nchini Guinea waliopindua serikali ya Rais Alpha Conde wameahidi kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa ambao wamekuwa gerezani chini ya utawala wa Conde.

Wanajeshi hao pia waliahidi kufanya mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali mpya ya mpito ya umoja wa kitaifa lakini hawajatoa maelezo zaidi ikiwemo tarehe.

Hayo yakijiri, kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Cellou Dalein Diallo alisema kwamba yeye pamoja na chama chake wako tayari kushiriki katika mchakato wa mpito wa kisiasa nchini humo kufuatia mapinduzi hayo.

Diallo mwenye umri wa miaka 69 aliliambia shirika la Habari la Reuters kwamba watatuma wawakilishi kwenye mchakato wa kuirejesha nchi katika mfumo wa utawala wa kikatiba.

Kikosi maalum cha jeshi kinachoongozwa na kanalii Mamady Doumbouya kilichukua madaraka katika taifa hilo maskini la Afrika magharibi na kumkamata rais, kitendo kilicholaaniwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa.