FLORIDA, Marekani
BONDIA, David Haye, amerejea ulingoni kwa kishindo baada ya kumtwanga, Joe Fournier kwa pointi kwenye pambano kali lililopigwa huko Florida.
Bingwa huyo wa zamani wa uzani wa ‘cruiser’ na uzani mzito, alirejea baada ya kustaafu kwa miaka mitatu, akiwa na umri wa miaka 40 alirejea ulingoni dhidi ya rafiki yake wa zamani kwenye pambano waliokubaliana wakati wa likizo huko Mykonos.
Kwa muda wa raundi nane, Haye, aliweza kumuweka Fournier pembeni na mara moja akamdondosha chini.
Mapigano yake mawili ya awali, mnamo 2017 na 2018, alipoteza dhidi ya Tony Bellew ambapo majeraha yalikuwa yakichangia pa kubwa katika kupoteza mapambano hayo.
Ngumi ya mwishoni mwa duru ya kwanza kutoka kwa Haye ilimuondoa Fournier mchezoni na kumdondosha sakafuni. Waamuzi walifunga pambano hilo kwa niaba ya Haye (79-72, 79-72, 80-71).(AFP).