NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuzitatua changamoto mbali mbali zinazolikabili jiji la Zanzibar.

Hemed alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara katika maeneo yanayozunguka nyumba za maendeleo Michezani zilizopo mkoa wa Mjini Magharibi.

Alibainisha kuwa hajaridhishwa na muonekano wa maeneo hayo kutokana na hali mbaya akitolea mfano juu ya muonekano mbaya wa barabara, mitaro na suala la usafi katika maeneo hayo.

Alisema kuwepo kwa mitaro mibovu katika njia hizo inahatarisha usalama wa wananchi na afya za watoto wanaocheza na kupita katika mazingira hayo.

Akigusia suala la maji safi na salama, Hemed aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo kuwa serikali ya awamu ya nane ina mkakati utakaohakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa muda wote bila ya udhia wowote.

Kuhusu wananchi wanaokaa katika nyumba za maendeleo Michezani, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar kuhakikisha nyumba hizo wanapewa wananchi wanaostahiki bila ya upendeleo.

Alisema azma ya muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, marehemu mzee Abeid Amani Karume kujenga nyumba hizo ni kuwapa makaazi bora wananchi wanyonge wa Zanzibar.

Akijibu malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kuhusiana na upigaji wa miziki kwa sauti ya juu majumbani, Hemed aliwaagiza masheha kukaa pamoja na mkuu wa wilaya kuweka utaratibu mzuri utakaoridhiwa na wengi ili kuhakikisha wananchi hawabugudhiwi na kadhia hiyo.

Katika ziara hiyo, Hemed alikasirishwa na tabia ya wananchi kuvunja sehemu ya jumba namba 10 na kulitumia eneo hilo lisilo rasmi kwa matumizi ya utupaji taka.

Aidha, aliuagiza uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuchukua hatua ya haraka kutengeneza barabara ya kituo hicho, ili kurahisisha wananchi kuweza kufika kituoni hapo bila ya kikwazo chochote.

Nao wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na kukithiri kwa uchafu katika maeneo hayo kunakosababishwa na usimamizi mbaya na watendaji wa baraza la Manispaa.

Aidha, walisema kumekuwepo na tatizo la watu wanaojitokeza kufungua redio majumbani kwa sauti za juu jambo linalosababisha kero kwa wakaazi wa maeneo hayo.

Wananchi hao walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kwamba wanasikitishwa na harakati zinazoendeshwa katika maeneo ya viwanja vya Mnazimmoja hali inayosababisha kuharibiwa kwa viwanja hivyo, huku ikisababisha kupotea kwa lengo lililoasisiwa na muasisi wa Taifa la Zanzibar, marehemu Sheikh Abeid Amani Karume

Wakijibu changamoto za wananchi viongozi walioambatana na Makamu wa Pili wa Rais katika ziara hiyo walisema kumekuwepo kwa tatizo la ukiukwaji wa taratibu zinazofanywa na wakaazi wa nyumba hizo ikiwemo changamoto ya ulipaji wa kodi, ujenzi usiofuata taratibu unaosababisha kuharibu miundombinu ya kupitishia maji.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea kituo cha Afya Rahaleo ambapo ameridhishwa na huduma zinazotolewa kituoni hapo.

Akizungumzia changamoto zinazokikabili kituo hicho, Daktari dhamana wa kituo Ashura Miraji Mpatani alisema kituo kinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa eneo pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji kutoka katika laini ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).