Aitaka iwashughulikie wagushi nyaraka

NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani kuweka utaratibu mzuri utakaowaondoshea usumbufu wa kupatiwa huduma wananchi wanaofika kupatiwa huduma katika taasisi hiyo.

Hemed alieleza hayo jana katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Mwanakwerekwe wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kuangalia namna wananchi wanavyopatiwa huduma katika taasisi hiyo.

Alisema wananchi wengi wanafika katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma ambazo wanazilipia, hivyo lazima wawekewe utaratibu mzuri ili wapate huduma hizo vizuri na serikali ipate mapato.

Akizungumzia matumizi ya nyaraka feki katika kupata huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo, Makamu huyo alimuagiza mkurugenzi mkuu mamlaka ya usafiri na usalama barabarani kuchukua hatua kali dhidi ya watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo.

Alisema ili kuvikomesha vitendo vya kughushi na matumizi ya nyaraka feki, ni vyema watu watakaobainika wakachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Hemed aliwataka wananchi wanaofika kupatiwa huduma katika mamlaka hiyo kuwa waaminifu na kuachana na vitendo vya utapeli ikiwemo kughushi nyaraka za serikali.

Makamu huyo alimuagiza mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo kuangalia namna bora ya kuimarisha ulinzi katika eneo la maegesho ya gari kwa kufunga kamera za usalama ili kudhibiti uhalifu unaojitokeza mara kwa mara.

Akijibu baadhi ya changamoto zilizotolewa na wananchi, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Haji Ali Zubeir alisema mamlaka anayoisimamia inachukua hatua kwa wanaokiuka taratibu ili kuondosha vitendo vya kihalifu ikiwemo kughushi nyaraka feki za leseni.

Alieleza kuna jitihada kubwa zinazochukuliwa na mamlaka katika kusimamia sheria kwa wanafunzi wanaojifunza udereva kwa kutumia gari za ‘manual’ badala ya ‘automatic’ ili kuwajengea umahiri wanafunzi hao na kupunguza ajali.