NA KASSIM ABDI, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza taasisi ya Tony Blair kwa kazi nzuri inayoifanya kutokana na michango na misaada ya kimaendeleo wanayoitoa kupitia sekta mbali mbali.
Hemed alitoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa taasisi hiyo waliofika ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kubadilishana mawazo.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaridhishwa na jitihada zinazochukuliwa na taasisi ya Tony Blair inayosaidia sekta tofauti ikiwemo afya, miundombinu ya mawasiliano na masuala mengine ya kijamii.
Makamu wa Pili wa Rais aliwaeleza watendaji hao kuwa, kwa sasa serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk. Mwinyi katika kuimarisha uchumi wake imeelekeza nguvu zake kupitia sekta ya uchumi wa buluu unaojumuisha mambo mbali mbali kama vile uvuvi, utalii pamoja na nishati ya mafuta na gesi.
Akizungumzia juu ya suala hilo la ukuzaji wa uchumi, Hemed aliiomba taasisi hiyo kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuwawezesha wananchi na watendaji wake kwa kuwapatia mafunzo yatakayosaidia kuwajengea uwezo.
Aliwaomba watendaji hao kutoka taasisi ya Tony Blair kutoa kipaumbele maalum kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utalii pamoja na sekta nyengine kwa kuweka mifumo itakayounganisha baina ya sekta moja na nyengine ili kujenga mfumo imara wa kuimarisha utendaji wa kazi za kila siku.
Alifafanua kwamba, kufanikiwa kwa kuimarisha mifumo ya utendaji kazi itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto tofauti ikiwemo kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
Alisema, serikali ya mapinduzi Zanzibar imedhamiria kuimarisha sekta ya usafiri kwa kuimarisha bandari zake na viwanja vya ndege pamoja na kuimarisha uwekezaji kupitia ujenzi wa viwanda.
Naye mtendaji kutoka taasisi ya Tony Blair, Eden Getachew alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kupitia mazungumzo hayo na vipaumbele alivyovieleza taasisi ya Tony Blair itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na serikali na kuangalia namna bora kwa ajili ya utekelezaji wake.