KASSIM SALUM, OMPR
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmshauri Chama Cha Mapinduzi Kuu ya CCM Taifa, Hemed Suleiman Abdulla, ameupongeza Umoja wa Vijana wa mkoa wa Kusini Unguja kwa kuanzisha programU ya elimu ya inayolenga kuwasaidia wanafunzi ndani ya mkoa huo.
Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa pongezi hizo katika uzinduzi wa programu hiyo inayotambulika ‘kuza ufaulu’, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha Walimu Dunga, wilaya ya Kati Unguja.
Alisema suala la kukuza ufauli kwa wanafunzi ni jambo la msingi ikizingatiwa kuwa mkoa wa Kusini Unguja kitakwimu ni mkoa ambao matokeo yake hayaridhishi ndani ya miaka miwili mfululuzo.
Alieleza matarajio ya programu hiyo ni kuleta mabadiliko endelevu ambayo itatoa fursa kwa vijana wanaoendelea na masomo yao hasa ya katika elimu ya sekondari kuweza kukuza uelewa wao wa masomo na hatimae kuweza kuwa mfano kwa taifa katika ufaulu wao.
Alisema umefika wakati sasa kwa viongozi wa CCM katika ngazi zote kutoa mashirikiano ya kila hali ili kuhakikisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukuza elimu kwa hatua ya kupunguza ziro na kukuza ufaulu inaweza kufikiwa.
Alisema si jambo la kuridhisha kwa mkoa huo kuwa ni wa mwisho kielemu ukizingatia katika masuala mengine mbali mbali Mkoa huo ni wa kupigiwa mfano hasa uwepo wa nyenzo za kutosha kushawishi watoto kuweza kufanya vyema kwenye masomo yao.
Akigusia kuhusu malezi Hemed alieleza ni vyema kushirikiana pamoja katika malezi ili vijana waweze kufikia malengo yao ya kutafuta elimu.
Pamoja na mambo mengine, Hemed aliwataka voingozi wa chama na serikali kuelekeza nguvu zao katika kusaidia kukuza sekta ya elimu ili kuisaidia Serikali katika kuwahudumia vijana hao.
Alieleza kuwa, serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, imeweka mipango thabiti katika kuinua sekta ya elimu nchini ili wananchi wake waweze kupata elimu bila ya kikwazo chochote.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa Kusini Unguja, Muhamed Ali Muhamed alisema kuanzisha programu hiyo inatokana na hali ya elimu kushuka ndani ya mkoa huo.