KATIKA ujenzi wa uchumi wa kisasa kwenye nchi mbalimbali ulimwenguni, sekta binafsi huwa na mchango muhimu na wa kipekee hasa kwenye urahishaji utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi.

Zanzibar kama nchi nyengine ulimwenguni inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika uchangiaji wa ukuaji uchumi, ndio maana serikali sio tu ina mashirikiano ya karibu mno na sekta hiyo, pia inaiwekea mazingira mazuri ya kutekeleza vyema majukumu yake.

Sekta binafsi ni eneo pana sana ambalo linajumuisha kampuni zenye mitaji mikubwa iliyowekezwa ambapo hutoa huduma za kimataifa, eneo la kikanda na hata eneo la kitaifa, pia inajumuisha wajasirimali wadogo.

Kampuni zote kubwa zilizofikia kiwango cha kimataifa unazozijua, wamiliki wake hawakulala na kuamka wakijikuta wasimamia miradi mikubwa, bali walianza kazi tangu msingi, wakasimamia hadi majina yao na kampuni zao kufikia hatua ya kutajika ulimwenguni kote.

Hata hapa Zanzibar baadhi ya watu unaowafahamu kuwa ni matajiri ukihadithiwa historia zao utabaini kuwa wamepitia vikwazo vingi, wamechupa milima na mabonde, mwishowe wamefikia malengo.

Tunachotaka kukizungumza hapa ni wajasirimali wetu hasa wale wadogo walioenea katika maeneo mbalimbali wakijishughulisha na utoaji wa huduma katika jamii.

Kwanza kabisa tuchukue fursa hii kumpongeze Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa hatua anazozichukua za kuwaimarishia mazingira mazuri wajasirimali wadogo hapa Zanzibar.

Moja ya kilio kikubwa alichokigundua Dk. Mwinyi wakati alipofanya ziara ya mikoa na wilaya zote za Zanzibar, ni rundo la malalamiko na masikitiko ya wajasirimali.

Tunathubutu kusema kuwa hatua aliyoichukua Dk. Mwinyi ya kulizindua zoezi la kuwapatia vitambulisho maalum wajasirimali wa Zanzibar alilolifanya hivi karibuni ni sawa na kuwafungulia mlango wa kuelekea kwenye mafanikio.

Umuhimu wa vitambulisho hivyo ni kwamba serikali imewarasimisha na kuwatambua rasmi, hali ambayo itaiwezesha kujua wapo wangapi na wanajishughulisha na kazi zipi.

Kwa sababu serikali inawatambua rasmi na kwasababu inajua shughuli wanazozifanya, hakuna sababu kwa wajasirimali hao kuwezeshwa zaidi hasa suala la kupatiwa mikopo itakayowafanya wapige hatua kubwa zaidi kwenye uzalishaji na kuongeza mitaji.

Katika hotuba ya ufunguzi wa zoezi hilo la utoaji vitambulisho, Dk. Mwingi alibainisha serikali itatenga bilioni 50 na kuzishawishi benki zitenge bilioni 50, ambazo zitaekelekezwa katika utoaji wa mikopo kwa wajasirimali.

Hatua ya wajasirimali kuwa na vitambulisho itawaondoshea adha ya mrefu iliyokuwa ikiwakabili wajasirimali wa Zanzibar ya kila siku ama kila mwezi kutakiwa wakalipe ushuru katika taasisi na mamlaka mbalimbali.