JANGA la ugonjwa wa corona ambalo linakaribia miaka miwili sasa tangu liliopoibuka duniani na kuifika Tanzania, kwa kiasi kikubwa limeathiri sekta ya utalii na uwekezaji ambazo kwa Zanzibar zina umuhimu wa kipekee kiuchumi.

Wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na janga hilo ingawaje kunapambazuka taratibu kwa kupungua ugonjwa wa corona hasa baada ya kugunduliwa kwa chanjo, nchi kadhaa zimeanza mikakati ya kuifufua upya sekata ya utalii.

Hanapa shaka utalii ni sekta inayozingatia zaidi utoaji wa huduma, hivyo ili sekta hiyo iweze kuwavutia wageni wengi kutoka nje ya nchi, lazima nchi iwe na mipango mikakati ya kuvitangaza vivutio vilivyopo.

Haitoshi tu kuvitangza vivutio vilivyopo katika nchi, bali jambo muhimu kabisa katika mtangazo hayo lazima uoneshe na ubainishe upekee wa vivutio ulivyonavyo, ili vionekane tofauti na vivutio vilivyo katika nchi nyengine vinavyofanana na vilivyopo katika nchi yako.

Ukweli ni kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tuna kazi kubwa ya kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii, kwa sababu bado huko ulimwenguni havijaelewekwa hasa kwenye nchi zenye kutoa watalii wengi duniani.

Ulimwengu utakapopambazuka kwa kumalizika janga la ugonjwa wa corona, bila shaka watalii katika mataifa mbalimbali watapenda kutembelea nchi mbalimbali kutafuta hewa safi baada ya kuchoshwa kukaa karantini kwa muda mrefu.

Kwa dhati kabisa tuchukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi wa mfano wa kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, rais Samia alianza kazi ya kurekodi vipindi maalum vya televisheni vilivyopewa jina la ‘ROYAL TOUR’ ambavyo vitarushwa nchini Marekani na mataifa mengine kadhaa duniani.

Kwa bahati nzuri uzinduzi wa kurekodi vipindi hivyo umeanzia Zanzibar ambapo maeneo mbalimbali ikianzia Kizimkazi, Mji Mkongwe hadi vivutio vya utalii vilivyopo kisiwani Pemba.

Kwa upande wa Tanzania bara nako maeneo mbalimbali yamejumuishwa kwenye ‘ROYAL TOUR’ ikiwemo vivutio vilivyopo Bagamoyo pamoja na vivutio vilivyomo katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Katika jamii yetu wapo watu kwa hulka na maumbile yao hupinga kila kinachofanywa hata jambo liwe jema, zuri, lenye maslahi na faida kubwa, kwa hulka waliyojaaliwa nayo watapinga na kukejeli.

Kutokana na hali hiyo, hatushangai kusikia maneno ya pembeni pembeni baadhi ya watu wakipinga na kuponda hatua ya Rais Samia kurekodi vipindi vya ‘ROYAL TOUR’ vya kutangaza utalii na utamaduni wa kitanzania nje ya nchi.

Huwa tunajiuliza hawa wanaopinga wanafahamu umuhimu na faida ya muda mrefu kiuchumi ambayo nchi yetu itanufaika kutokana na hatua ya Rais Samia kurekodi vipindi vya ‘ROYAL TOUR’?

Utalii ni biashara yenye faida kubwa duniani, hivyo hata matangazo ya sekta hiyo kwenye vyombo vya kimataifa yanahusisha gharama kubwa, kwanini Rais aache kutumia fursa hiyo ambayo ingetulazimu kama nchi kutumia mabilioni ya dola?

Wahenga wanasema ‘Biashara itangazwayo ndiyo itokayo’, itoshe kuwaeleza wananchi kwamba pasi na kuvitangaza vivutio vyetu ili kuvutia wageni, tutaendelea kubakia na vivutio hivyo pasi na faida yoyote.

Sisi tunaamini hatua ya Rais Samia kurekodi vipindi vya ‘ROYAL TOUR’ni kwa faida na maslahi mapana ya nchi yetu, tuvute subira muda utatoa majibu ya haya.