NA SAIDA ISSA, DODOMA

TANZANIA inakabiliwa na tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani na kwa takwimu zilizopo ni kwamba inakadiriwa kuwa na idadi ya hao imefikia 35,919, ambao wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika majiji na miji mbalimbali.

Hayo yamebainishwa wakati wa kikao kazi cha Makatibu Tawala Mikoa, Makamanda wa Polisi Mikoa na Wadau wanaohusika na masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kilichofanyika leo Jijini Dodoma.

Awali akifungua kikao hicho, katibu mkuu wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu alisema kuwa tafiti zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam ilibaini jumla ya watoto 6,393 ambao walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani.

Dk. Jingu alisema kuwa kundi hili ni kubwa na linapokuwepo katika jamii yoyote ni changamoto kwa Ustawi na Maendeleo ya Jamii husika kwani athari mojawapo ni watoto hao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Aidha alieleza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuweka mkakati na kuwa na mtizamo wa pamoja unaounganisha nguvu na rasilimali nyingine ili kumaliza tatizo hili kama sio kulipunguza kwa kiasi kikubwa.

Naye Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Shilungu Ndaki akiwasilisha taarifa ya Hali ya tatizo hilo nchini alisema Serikali imefanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuzuia ongezeko la watoto hawa na pia kutoa huduma ya msaada kwa watoto ambao wako tayari mtaani.

Pia alitaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kusimamia Kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kusimamia programu zinazolenga uchumi wa kaya na kutengeneza muongozo wa kuunganisha watoto na familia.

Ndaki alisema kwamba hadi mwezi Machi mwaka huu watoto 1005 waliokuwa mitaani wameunganishwa na wazazi wao hivyo kupunguza watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika miji na majiji.