NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

ASKARI  11 waliohusika katika shambulizi linalodaiwa la kigaidi lililotokea Agosti 25 mwaka huu mtaa wa Kenyata jijini Dar es Salaam, wamepewa vyeti vya hati za ujasiri na fedha shilingi 500,000 kila mmoja.

Akizungumza jana jijini hapa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muriro Jumanne Muriro alisema askari hao kwa mamlaka ya kisheria za uendeshaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Afande Inspekta Jenerali wa Polisi amewapa zawadi za vyeti vya ujasiri na pesa kwa kadri alivyoona inafaa.

Alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni miongoni mwa kazi ngumu tofauti na watu wanavyotazama la kulinda wananchi na mali zao.

“Kulinda wananchi wakiwa ndani ya nyumba zao au nje za ofisi zao au mahali popote walindwe pia na mali zao, hilo ni jukumu la askari polisi kwani anakula kiapo”, alisema.

Alisema askari kupoteza maisha sio hali ya kawaida pamoja na jukumu lako ukaamua kufa kwa ajili ya watu wengine.

Alieleza moja ya haki za msingi za kikatiba kila mtu kuishi lakini askari polisi yuko tayari kufa kwa ajili ya watu wengine wanaoishi, ambapo askari hao walipambana kuhakikisha kwamba madhara makubwa zaidi ya yale yaliyotokea hayatokei.

“Nani ambaye hafahamu kama mhalifu angeondoka na zile silaha zilizokuwa na magazine mbili na risasi 60 na risasi zingine zilizokuwepo”, alisema.

Aliwapongeza askari wa Polisi walioshiriki kwa kazi kubwa ya weledi waliyoifanya kwa sababu kama ingekuwa kazi ya ovyo kama watu wanavyobeza watu wangekufa zaidi, kama risasi hizo zingepigwa ovyo ovyo, wangekufa raia wengi.

Aliendelea kuwatia moyo askari majasiri ambao wameumia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, pamoja na familia za askari waliopoteza maisha kwa niaba ya kulinda watu, hizo ndio kazi za uaskari.

Alisema baadhi ya silaha ziliporwa na mhalifu aliyekuwa na viashiria vya kigaidi na askari watatu na mmoja wa kampuni ya ulinzi walipoteza maisha na askari wengine walipata majeraha.

Alisema katika tukio hilo walikuwepo askari  wengi ambapo wote walifanya kazi nzuri lakini askari 11 walifanya kazi ya ziada ya wengine.