KABUL, AFGHANISTAN

SHIRIKA la habari la Amaq lenye uhusiano na wanamgambo wa Islamic State, ISIL linasema kundi hilo lilitekeleza mashambulio ya mabomu dhidi ya Taliban katika mji wa mashariki mwa Afghanistan wa Jalalabad mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mfululizo wa mashambulio hayo yaliyotekelezwa mjini humo ulionekana kuilenga Taliban.

Vyanzo vya habari vya serikali ya jimbo vinasema mabomu hayo yaliua watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine 15, wakiwemo wapiganaji wa Taliban.

Shirika hilo liliripoti kuwa vyanzo vyake vya habari vinasema mashambulio mengi yaliyotekelezwa na wapiganaji wa kundi la Islamic State yaliua na kujeruhi wanachama 35 wa Taliban.

Kundi linaloshirikiana na Islamic State la nchini humo lilidai kutekeleza shambulio la bomu la kujitoa mhanga Agosti 26 karibu na uwanja wa ndege wa Kabul.Shambulio hilo liliua watu zaidi ya 100 wakiwemo wanajeshi wa Marekani.