NA ASIA MWALIM
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Japani Tanzania (JATA), Idriss Muslim Hija, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira ya kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili kujenga uchumi imara kwa taifa hilo.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua warsha ya uchumi wa buluu na muelekeo wake kwa maendeleo ya Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Fumba Zanzibar.
Alisema hatua hiyo ni kutokana na uwepo wa fursa mbali mbali zilizopo ndani ya bahari na vipaumbele vya uwekezaji chini ya uchumi wa buluu ikiwemo sekta ya uvuvi mdogo mdogo na bahari kuu.
Aidha alisema maamuzi ya uwekezaji katika uchumi wa bahari hapa nchini yamefikiwa kwa kutambua uwezo na mchango wa maliasili, rasilimali za pwani na baharini zinavyovizunguka visiwa vya Zanzibar.
Alisema katika kuhamasisha matumizi endelevu ya bahari kwenye suala la uzalishaji na upatikanaji wa ajira kwa wazanzibari, serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafanikiwa katika kutekeleza azma hiyo.
Mwenyekiti huyo alieleza dhana ya uchumi wa buluu, alisema serikali inafanya jitihada za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, ambapo mipango ya kununua vyombo vitakavyotumika kwenye aina hiyo ya uvuvi imekamilika sambamba na kutekeleza zoezi la kuwapatia vyombo vya kisasa na mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Alifahamisha kuwa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, imejikita katika kuimarisha masoko ya samaki yaliyopo pia kujenga masoko mapya sambamba na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya Zanzibar.
Akizungumzia sekta ya mafuta na gesi asilia, Dk. Hija alisema ni kiungo muhimu katika dhana ya uchumi wa buluu hivyo ni vizuri kujipanga katika kuinua rasilimali hiyo, kuzikaribisha kampuni za mafuta na gesi asilia zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini.
Aidha alisema utekelezaji wa dhana ya uchumi wa buluu hautawezekana bila ya kuwa na bandari za kisasa na zenye ufanisi wa hali ya juu, hivyo serikali imefikiria kujenga bandari kubwa katika maeneo ya Mangapwani ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika bandari ya Malindi hivyo ajira nyingi zitapatikana na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.