NA HUSNA MOHAMMED
KILA ifikapo Septemba 1 hadi 8 ya kila mwaka hujulikana kuwa ni siku ya kimataifa ya kisomo cha watu wazima duniani – International Literacy Day (ILD).
Siku hiyo inatokana na mkutano mkuu katika kikao cha 14 cha shirika la elimu, sayansi na utamaduni cha Umioja wa Mataifa yaani UNESCO mwaka 1966 kilichofanyika Tehran, Iran.
Tokea mwaka 1967 siku hiyo ya maadhimisho ya Elimu ya Watu wazima imekuwa ikifanyika duniani kote kila mwaka.
Pamoja na mambo mengine lakini lengo na madhumuni ya kuwakumbusha wananchi na jamii juu ya umuhimu wa kisomo cha watu wazima na elimu kwa ujumla kuwa suala la msingi, utu na haki ya kila mtu.
Pia siku hii huwatanabahisha na kuwasisitiza wananchi na jamii kutilia mkazo suala la elimu kwa maendeleo endelevu katika jamii ili kuelekeza juhudi katika mahitaji ya fani na ujuzi wa kazi bila ya kujali changamoto zilizopo.
Maadhimisho ya siku ya Elimu ya Watu Wazima kimataifa mwaka huu ni fursa kubwa ya kuelezea umoja na mshikamano na kuwa ni mwaka wa lugha za asili au lugha za kienyeji.
Maadhimisho ya siku ya Kisomo duniani kwa mwaka huu 2021 yanalenga katika “Kisomo Chenye Manufaa Kizingatie Uwiano wa Matumizi ya Kidigitali”. Kauli mbiu hii inatoa fursa ya kuangazia upya namna ya kuendeleza stadi za kisomo kwa kuzingatia uwiano wa kumshirikisha mwanakisomo katika matumizi ya kidigitali kwa kipindi hiki cha janga la corona ili kuleta maendeleo ya kiuchumi katika jamii na taifa kwa jumla.
Juma la wiki ya Elimu ya Watu Wazima duniani inaangalia na kutathmini namna ya kisomo cha watu wazima kinavyowanufaisha wale ambao hawakupata elimu ya lazima utotoni.