NA KIJA ELIAS, MOSHI
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania (JMT) na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Al had Mussa Salum, amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu kwenye Sensa ya majaribio ya Watu na Makazi inayotarajiwa, kwani ina faida kubwa kwa taifa ikiwemo uwekezaji pamoja na maendeleo.
Sheikh Al had Salum, aliyasema hayo jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Kamati Kuu ya Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Kilimanjaro, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Al had, aliwaomba viongozi wa dini kuwahamasisha waumini wa madhehebu yote kutoa ushirikiano kwa Serikali, ili utakapofika muda wa zoezi la sensa ya Watu na makazi waweze kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa, jambo ambalo litawezesha kuwafikia wananchi ili watambue umuhimu wa sensa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
“Sensa ya Watu na Makazi ni takwa la kisheria, jambo hili lipo hata katika dini zetu, kanisa au misikiti ni lazima lifahamu lina idadi ya waumini kiasi gani, hivyo hivyo na Serikali inataka kufahamu idadi ya wananchi ilionao,”alisema Al had Sheikh Salum.
Alisema Sensa ya watu na Makazi inasaidia kupata idadi kamili ya watu walio kwenye eneo husika hivyo hata mafungu ya fedha yanayotolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo yatatoka kulingana na idadi ya watu hivyo ni lazima wahesabiwe kwa ajili ya maendeleo.
Awali akifungua kikao hicho Kaimu Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Saidi Mtanda, aliwapongeza Jumuiya hiyo kwa kuweza kuisaidia serikali katika kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.