NA ABOUD MAHMOUD

WAZIRI wa Nchi Ofisi Makamu wa Pili Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed amesema serikali itafanya uchunguzi juu ya hoja ya udanganyifu wa kujipatia fedha kwa mfanyakazi wa kitengo cha damu salama ili haki ipatikane.

Dk. Khalid alisema uchunguzi utafanywa na mamlaka husika ili taarifa kamili zipatikane ambazo zitatumika kupitishwa maamuzi ya haki.

Aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha taarifa ya serikali kuhusu hoja ya udanganyifu wa kujipatia fedha kwa mfanyakazi wa kitengo cha damu salama.

Alifahamisha kwamba pamoja na yote yaliyobainika kamati maalumu ya wataalamu, serikali bado imeona ipo haja ya suala hilo kuchunguzwa kwa umakini mkubwa.

Alibainisha kwamba zipo taarifa kuwa matumizi ya hesabu za benki ya JUWADAHIZ kuingizwa fedha zinazoombwa kwa matumizi ya kitengo cha damu salama yalipata baraka za Wizara kupitia waziri aliyekuwepo wakati huo.

Hata hivyo alisema kupitia kadhia hiyo wizara ya Afya ilimpatia onyo la maandishi na kuelezwa kwamba pindipo akirejea makosa ya aina hiyo adhabu kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

“Muhusika alipewa uhamisho wa kikazi na kwenda kuendelea na kazi katika Idara ya Kinga na Elimu ya Afya”, alisema.

Sambamba na hilo alisema muhusika huyo alikuwa na utaratibu wa kuomba fedha na vifaa kila mwaka na baadhi ya taasisi zilizoombwa na kuingizwa fedha katika hesabu za Benki za JUWADAHIZ tokea mwaka 2018.

Kwa niaba ya kamati ya Kusimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa, mjumbe wa kamati hiyo Mtumwa Peya Yussuf, alisema kamati imebaini kukosekana kwa utaratibu wa kutekeleza jambo hilo katika hatua za awali ndani ya Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto.