NA AMEIR KHALID
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Khamis Juma, amezindua rasmi kamati mbali mbali zitakazohusika na maandalizi na kilele cha sherehe za tamasha la elimu bila malipo mwaka 2021.
Uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa wizara hiyo Mazizini, ambapo katika nasaha zake kwa wanakamati hao, aliwataka kufanya kazi kwa kujitolea ili tamasha hilo lifikie malengo yake.
Aliwataka kila mmoja kuhakikisha anafanya kazi kwa kujituma ili tamasha hilo lifanikiwe, kwa kuhakikisha wanajitolea bila ya kujali pesa.
Alisema tamasha la elimu bila malipo mwaka huu litakuwa na mabadailiko ya baadhi ya mambo, ikiwemo idadi ya wanafunzi watakaoshiriki, ambapo mwaka huu washindi wa kwanza na wa pili ndio watakaokweda kisiwani Pemba badala ya mshindi wa kwanza hadi watatu.
Aliwataka wajumbe hao kujipanga vyema kuonyesha utofauti wa matamasha yaliopita, kwa kuongeza baadhi ya mambo ambayo ni muhimu kujulikana, kwa kila taasisi kuonyesha nini inafanya.
‘’Tamasaha hili lisiwe la michezo pekee, vyema kila taasisi ndani ya wizara kuonyesha nini inafanya, kwani elimu ina nyanja pana sana hivyo vyema zote zikazingatiwa’alisema.