BERLIN, UJERUMANI

WAZIRI wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp- Karrenbauer anataka kupendekeza kuundwa kwa ujumbe huru na wa haraka wa kijeshi chini ya Umoja wa Ulaya baada ya uchaguzi nchini humo.

Katika toleo la Jumamosi la gazeti la Franfurter Allgemeine, Karrenbauer alisema kuwa anadhani kifungu cha 44 cha mikataba ya Ulaya kinatoa nafasi ya maamuzi ya pamoja ya Umoja wa Ulaya na utekelezaji wa operesheni za kijeshi za Ulaya kupitia miungano ya mataifa wanachama yanayotaka kufanya hivyo chini ya umoja huo.

Karrenbauer alisema kwamba wanatayarisha pendekezo kuhusu suala hilo ambalo linapaswa kuwasilishwa wakati wa mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba.

Kifungu cha 44 kinasema kwamba Baraza la Umoja wa Ulaya linaweza kutwika jukumu la kuandaa ujumbe wa kijeshi kwa kundi la mataifa wanachama yanaotaka kufanya hivyo na ambayo yana uwezo unaohitajika kwa ajili ya kuendesha operesheni kama hizo.