MADINA ISSA NA TATU MAKAME

MKUU wa wilaya ya Kaskazini ‘B’, Hamid Seif Said, amewataka watendaji wa Wilaya, Baraza la Mjii na Masheha kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo ya utumishi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizunguma mara baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Mji kaskazini ‘B’ Kinduni, alisema ili serikali itekeleze miradi mbalimbali ya kimkakati ipo haja kwa watumishi hao kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo.

Hivyo, aliwaomba wafanyakazi na watendaji wengine kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano ili lengo la kuwafikishia wananchi huduma zilizokuwa bora zifikiwe.

“Tuendelezeni mashirikiano tuliyokuwa nayo ili maendeleo yaweze kufika kwa wannachi wetu ambapo ndio msimamo wa serikali ya awamu ya nane kuwafikishia wannachi huduma zilizokuwa bora” alisema.

Mapema aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Aboud Hassan Mwinyi, alisema miongoni mwa mambo aliyoyatekeleza katika uongozi wake ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi kutoka migogoro 106 aliyoipokea hadi kufikia migogoro 54 ambayo bado haijatatuliwa.

Alisema wilaya ya Kaskazini ‘B’ ina fursa nyingi za ajira ikiwemo ujenzi wa bwawa la umwagiliaji maji Kisongoni, uwekezaji wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Bumbwini pamoja na sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inasaidia kuondoa tatizo la upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana.

Hata hivyo, Aboud alitaka jamii kusimamia vijana wao katika maadili mazuri na kuachana na tabia ya kuchagua kazi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ndani ya wilaya hiyo.

Sambamba na hayo, aliwaomba watendaji wa wilaya hiyo kumpa ushirikiano Mkuu huyo ili kazi ziweze kwenda sawa kama ilivyokuwa wakati akiwa mkuu wa wilaya hiyo.

Akitoa shukran kwa niaba ya watendaji wenzake, Alhaji Bakari Haji, aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mkuu huyo wa wilaya ili kufikia malengo ya serikali.