NAIROBI, KENYA
SHIRIKA la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeilaumu serikali ya Kenya kwa kushindwa kuchukua hatua za kukabiliana na ongezeko la vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Vitendo hivyo vingi viliripotiwa kutokea wakati wa maambukizi ya corona hususan wakati wa utekelezaji wa zuio la kubakia majumbani ili kuzuia maambukizi ya COVID-19.
HRW imedai katika ripoti yake kwamba serikali ya Kenya ilishindwa kuhakikisha kuwa wanawake wanapata huduma za kiafya, kiuchumi na za kijamii kufuatia vizuizi mbalimbali vilivyowekwa ambavyo vimeathiri shughuli zao.
Ripoti inasema kulikuwepo na ongezeko kubwa la asilimia 301 ya simu zilizoripoti unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana katika wiki mbili za kwanza za karantini kati ya mwezi Machi na Aprili 2020.
HRW ilisema,wakati tafiti za awali zilionyesha kuwa visa vya unyanyasaji wa kijinsia vinaongezeka wakati wa dharura za kiafya,serikali ya Kenya inapaswa kubuni mpango sawa wa wakati wa dharura ya afya wa wakati wa ugonjwa wa COVID-19.
Shirika hilo limeongeza kuwa,utafiti mwengine juu ya unyanyasaji wa kijinsia pia ulionyesha kuwa miundo na sera za sasa za serikali ya Kenya hazitoshi kutoa suluhisho la ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wakati wa dharura kama hizo.
Ripoti hiyo ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ilichapishwa kwa kutegemea mahojiano 26 yaliyofanywa kati ya mwezi Juni mwaka jana na Februari mwaka huu ambapo watu 13 waliohojiwa ni manusura wa unyanyasaji wa kijinsia.
HRW limetaja aina mbalimbali za unyanyasaji huo wa kijinsia dhidi ya wanawake na mabinti kama kubakwa, kupigwa, kufukuzwa nyumbani, kulazimishwa kuolewa na kuwalazimisha kukeketwa.