PARIS, UFARANSA

KESI ya mashambulizi ya kigaidi ya Paris ya mwaka 2015 imeanza kusikilizwa.

Wanamgambo wa Islamic State waliua watu 130 walipoingia kwenye ukumbi wa tamasha, migahawa na vituo vyengine ndani na karibu na mji mkuu huo wa Ufaransa Novemba 13, 2015.

Wengi wa washambuliaji hao walifariki katika miripuko ya mabomu ya kujitoa mhanga na kufyatuliana risasi na polisi.

Salah Abdeslam anayeaminika kuwa manusura pekee, alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya ugaidi.

Abdeslam, alionekana kwenye chumba maalum cha mahakama kilichoimarishwa usalama mjini Paris.

Jaji mkuu alipomuuliza taaluma yake, Abdeslam mwenye umri wa miaka 31 alisema aliachana na taaluma zote ili awe mpiganaji wa Islamic State.

Usikilizaji wa kesi hiyo unatarajiwa kuendelea hadi mwezi Mei mwakani.Wengi wanafuatilia kuona ni kwa kiasi gani taswira kamili ya mashambulizi hayo itafichuliwa.