LONDON, England
KLABU ya Tottenham Hotspurs imeripotiwa kumpa kiungo wa AC Milan, Franck Kessie, mkataba wenye thamani ya pauni milioni nane kwa mwaka kumshawishi ahamie Ligi Kuu ya England msimu ujao wa joto.

Mkataba wa sasa wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 huko San Siro unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwakani, na klabu kadhaa pamoja na Spurs, Chelsea na Liverpool, zinaendelea kuihitaji huduma yake.

Ripoti ya hivi karibuni iliwataja Chelsea kuwa wamewasiliana na wawakilishi wa Kessie ili kuweka mambo sawa na mkataba mezani, ambao ungekuwa na thamani kubwa zaidi kuliko mkataba wake wa sasa huko Milan.

Kwa mujibu wa chanzo cha Calciomercato, Spurs pia inamtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, wamewasilisha kandarasi yenye thamani hiyo wakiwa na matumaini ya kumshawishi aende Spurs.

Kessie alikuwa na kampeni nzuri ya 2020-21 akiwa na klabu yake ya sasa huko Italia, akifunga magoli 14 na kuchangia magoli sita katika mechi 50 za michuano yote.(AFP).