RAMALLAH, PALESTINA
KIJANA mmoja wa Kipalestina ameuawa na makumi kujeruhiwa siku ya Ijumaa katika mapigano kati ya waandamanaji wa Palestina na wanajeshi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi, madaktari na mashuhuda walisema.
Mohammed Khbeisa, mwenye umri wa miaka 28, aliuawa na wanajeshi wa Israeli wakati wa mapigano katika kijiji cha Beita, karibu na mji wa Nablus kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, Wizara ya Afya ya Palestina ilisema katika taarifa.
Mashuhuda walisema kwamba waandamanaji wengi wa Wapalestina waliandamana katika kijiji hicho wakipinga upanuzi wa makazi ya Israeli na kutwaliwa kwa ardhi za Wapalestina.
“Waandamanaji walichoma matairi, wakipeperusha bendera za Wapalestina, waliimba misemo dhidi ya Israeli na kurusha mawe kwa wanajeshi wa Israeli waliokaa kwenye kituo cha Israeli karibu na kijiji, wakati wanajeshi wa Israeli walipiga mabomu ya machozi, risasi za moto na risasi za chuma zilizotiwa na mpira kuwatawanya waandamanaji”, walisema mashuhuda.
Chama cha Red Crescent cha Palestina kilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba watu kadhaa walijeruhiwa na risasi za mpira na wengine walipata shida ya kupumua baada ya kuvuta hewa ya mabomu ya machozi.
Mapigano katika kijiji hicho yamekuwa yakiendelea kwa karibu miezi minne kufuatia kuanzishwa kwa jeshi la Israeli katika sehemu za ardhi za kijiji zinazomilikiwa na wakaazi wake.Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ililaani mauaji ya Khbeisa.