LONDON, England

THOMAS Tuchel, Kocha Mkuu wa Chelsea amesema anafikiria kwamba bado kuna nafasi ya mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane kujiunga na Manchester City hivi karibuni.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu England ambao ni City walikuwa kwenye hesabu ndefu za kuipata saini ya Kane, ila mambo yalibuma baada ya mchezaji huyo kubadili maamuzi na kuamua kubaki ndani ya Tottenham.

Ilikuwa ni Mei,2020 nyota huyo alifunguka kwamba anahitaji kupata changamoto mpya na timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi ya kumpata ilikuwa ni City inayonolewa na Kocha Mkuu, Pep Guardiola.

Pia hata Chelsea nao walikuwa wanahitaji saini ya Kane ambaye alishinda kiatu cha ufungaji bora msimu uliopita nao walikwama wakaishia kuipata saini ya Romelu Lukaku ambaye alikuwa anakipiga ndani ya Inter Milan.

Tuchel alipouliziwa kuhusu ishu ya Kane alisema:”Nadhani kuna jambo ambalo linaweza kutokea kwa wakati ujao, kwetu sisi hatukuwa na mpango wa kufanya hivyo na sijasema kwamba tunahitaji kumnunua mchezaji huyo

“Ninadhani kwamba kuna jambo ambalo lingetokea ikiwa angepata nafasi ya kwenda Manchester City hivyo kuna mambo ambayo yapo,”