WASHINGTON, MAREKANI
MBUNGE wa Kongresi ya Marekani amebuni muswada unaopiga marufuku uuzaji wa silaha za nchi hiyo kwa tawala za Saudi Arabia na Israel.
Alexandria Ocasio-Cortez aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba amefanya mabadiliko katika muswada wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022 ambayo yanapiga marufuku uuzaji wa baadhi ya silaha kwa Saudi Arabia kwa sababu ya faili la mauaji yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala huo, Jamal Khashoggi.
Pia alipiga marufuku ya kuuza silaha hizo kwa utawala wa Israel kwa kushambulia jengo la vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza.
Marekebisho hayo pia yanazuia kuuzwa baadhi ya silaha kwa serikali ya Colombia kwa sababu ya kuwakandamiza waandamanaji.
Iwapo yatapasishwa, marekebisho hayo yatazuia kuuzwa silaha makini kwa utawala wa Israel ikiwemo shehena ya silaha za JDMA yenye thamani ya dola milioni 735.
Muswada huo ulimkasirisha sana balozi wa Israel nchini Marekani na balozi mwakilishi wa utawala huo katika Umoja wa Mataifa.