Msiba usiosahaulika kwa Wazanzibari, iliua zaidi ya watu 200

Makumi ya watu hawakuonekana hadi sasa

NA MWANDISHI WETU

USIKU wa kuamkia kama jana miaka 10 iliyopita ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Zanzibar.

Hii inatokana na msiba mkubwa ulioacha huzuni na majonzi yasiyoelezeka baada ya meli ya Mv Spice Islander kuzama katika mkondo wa Nungwi ikiwa safarini kutoka Unguja kwenda Pemba.

Ajali hiyo ilikuwa ya kwanza kubwa katika bahari ya Zanzibar na hapana takwimu sahihi za watu waliopoteza maisha, lakini inakisiwa zaidi ya 1,000.

Vile vile palitokea hasara kubwa ya bidhaa, vitu vya abiria na mabaharia na meli kuzama.

Baaadhi ya watu walibahatika kuokolewa, lakini wapo ambao miili yao haikupatikana hadi sasa.

Makala hii haina lengo la kukumbusha huzuni na simanzi miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla huu ni msiba wa taifa. Na kwamba kumbukumbu itaendelea daima hasa kwa jamaa wa wahanga wa ajali hiyo.

Lakini miongoni mwa majukumu ya vyombo vya habari ni kukumnbusha masuala kama haya kama tahadhari ya kujikinga na ajali za aina hio zisitokee tena.

Taarifa mbali mbali, ikiwemo ya uchunguzi wa ajali hiyo, zilieleza kuwa mali nyingi zilipotea na hadi sasa bado haijajulikana thamani kamili.

Wapo wanaokisia watu waliokufa ni 1,370, idadi ambayo inaonesha ukubwa wa msiba huu katika historia ya usafiri wa majini, nchi kavu na anagani katika visiwa hivi vya Bahari ya Hindi, mashariki ya bara la Afrika.

Chambilecho maneno ya wahenga, ‘Ukupigao ndio ukufunzao’, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa wakati huo Dk. Ali Mohamed Shein (mstaafu) ilianza juhudi za uokozi mara tu zilipopatikana taarifa ya hio meli kuzama katika eneo la Nungwi na kuanzisha vituo vya matibabu, kupokea maiti na majeruhi.

Kwa mujibu ripoti ya tume ya iliyochunguza kuzama kwa meli hiyo iliyoongozwa na Jaji Abdulhakim Ameir Issa, iliyotolewa mwezi wa Februari 2012, ilieleza kuwa idadi ya maiti zilizopatikana na kuzikwa zilikuwa 243, huku watu 941 wakiokolewa wakiwa hai.

Tume iligundua kuwepo upakiaji wa abiria kupindukia uliotokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za usafiri baharini.

Vile vile kulikuwepo uwekaji mbaya wa mizigo, matatizo ya kiufundi yaliofanya kiwango cha upakiaji mizigo kisijulikane na uzembe wa nahodha.

Tume hiyo ilisema licha ya meli kuwa na uwezo wa kupakia abiria 620, meli hiyo ilikuwa ilipakia abiria 2,470, karibu mara nne zaidi ya uwezo wake.

Aidha tume ilisema ubovu wa meli ulijulikana tokea mwezi Julai, miezi miwili kabla ya meli kuzama baada ya ukaguzi uliofanywa na taasisi ya usalama wa bahari, lakini bado meli hiyo ilipewa leseni.

Taarifa iliongeza kuwa ulikuwepo mnyororo mrefu wa watu waliokuwa na dhamana lakini walishindwa kufanya wajibu wao.

Hawa ni pamoja na maafisa wa meli, bandari, polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao walidaiwa kupokea fedha ili kupenyeza abiria, jambo ambalo ndio liliosababisha maafa.

Tume ilipendekeza watu kadhaa washtakiwe na ilitaja makosa iliyoona yaliyowahusu na polisi waliwatia mbaroni watu kadhaa.

Kwa bahati meli hiyo ilikuwa na bima, lakini sio pamoja na mizigo. Hii ilisaidia kuwalipa jamaa za watu waliokufa na tume ilipendekeza angalau kiwango cha shilingi 10,000,000 kwa kila aliyefariki au kupotea.

Katika mapendekezo yake tume hiyo ilitaka hatua za kisheria na nidhamu kwa baadhi ya waliohusika na msaada kwa waliopoteza ndugu, jamaa na mali zao na yote haya yalitekelezwa.

Mwaka mmoja baadaye, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Rashid Seif, alisema serikali ilijipanga kuhakikisha maafa kama hayo hayatokei tena.

Lakini kabla haijamalizika miezi meli nyengine ya Mv Skagit ilizama wakati ikitokea Dar es Salaam kwenda Unguja na zaidi ya watu 100 kupoteza maisha.

Hakuna jicho lenye huruma lililojizuia kutokwa na machozi kwa msiba huu mkubwa kwa Zanzibar na watu wa Visiwani waliungana katika kipindi kile kigumu cha misiba, hasa ya mv Spice iliyouwa watu wengi zaidi.

Hapana shaka huu ulikua mtihani kutoka kwa Mungu, lakini kama ilivyogundua tume ya uchunguzi uzembe wa mkururo wa wahusika hauwezi kutengwa kando kwenye maafa makubwa kama haya.

Sabri Juma ambaye alipompoteza mke wake katika ajali hio alihisi kama nyumba yake wakati ule ilikuwa ikimzomea kila alipongia huku akiwa na kumbukumbu za mke wake.

Nae Kijana mmoa aliyejitambulika kwa jina moja la Ali maarufu Maafa anaeishi Fuoni, ambae aliokoka kwenye ajali hiyo, alisema hataisahau kamwe ajali hiyo na hadi sasa kuweko hai baada ya kuokolewa.

“Ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye alieniokoa kwa sababu hali ilikuwa ngumu nilipata kushika godoro mimi na wenzangu tukaokolewa”, alisema.

Alisema hadi leo watu wanamwita maafa kutokana na kupata maafa hayo ya kuzama baharini kiasi kwamba alisema ikiiona tu bahari hukumbuka mkasa uliompata.

MAOMBI NA SALA WAKATI WA AJALI

Serikali ilizigawa kwa waathirika na jamaa za marehemu fedha zilizokusanywa kama michango.

Viongozi wengi wa dini na wa serikali waliohudhuria sala maalum ya kuwaombea waliopoteza maisha yao baada ya kuzama kwa meli ya mv Spice Islander. Sala ilifanyika katika viwanja vya Maisara ambapo maiti ziliwekwa ili kutambuliwa na ndugu jamaa na marafiki.

Serikali ilitoa eneo la Kama ili kuzikiwa baadhi ya maiti waliokufa katika ajali ya Spice Islander.

KIKOSI MAALUM CHA KUZUWIA MAGENDO (KMKM)

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kikosi cha KMKM hasa katika uokozi wa majini, ilisema Serikali imekiongezea nguvu kikosi hicho kiasi kwamba hadi sasa katika shughuli zauokozi majini ainatia moyo ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Taarifa zilisema kikosi hicho kimeongezewa nguvu kwa kukipatia vifaa vya kisasa, zikiwemo boti zinazokimbia kwa kasi.

Aidha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa imeshirikiana na vikosi vya ulinzi na kuimarisha ujenzi wa vituo vya uokozi Nungwi na Kibweni (Unguja) na Mkoani, Pemba. Vituo hivi vimepatiwa vifaa vya uokozi.

“Vituo hivi vimefungwa vifaa maalum vya mawasiliano na kuweza kuwa na mifumo mitatu ijulikanayo kwa majina ya VMS, Sea Vision na Find Ship”, alisema.

Sambamba na hilo, lakini mifumo hii inasaidia kupata taarifa kutoka kwenye vyombo vya baharini  kwa urahisi na wananchi na kuimarisha mashirikiano baina ya KMKM na Mamlaka ya usafirishaji baharini (ZMA), MRCC na vyombo vya ulinzi vya Jamuhuri ya Muungano, hususan Jeshi la Wananchi Tanzania na Uhamiaji.

Aidha kwa sasa vituo kunahakikisha upatikanaji wa huduma za uokozi, uzamiaji na ulinzi wa nchi na kuepusha majanga ya uzamaji wa vyombo baharini na athari za maisha ya wananchi.

Mpaka sasa kikosi hicho kimekuwa na mabadiliko makubwa, ikiwemo kudhibiti magendo sambamba na suala la maafa ya baharini.

Katika kumbukumbu hiyo tunawaombea dua na mapumziko mema peponi wale wote waliofariki kwenye ajali hiyo sambamba na waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki Mwenyezi Mungu kuwapa subira.