NA MZEE GEORGE

WANANCHI wa Mtoni Kijundu shehia ya Mtoni wilaya ya Magharibi ‘A’ wameiomba serikali kuwafikishia huduma muhimu za kijamii ili kuwaondosheha changamoto zinazowakabili.

Wananchi hao wametoa ombi hilo katika mkutano maalumu na uongozi wa wilaya ya Magharibi ‘A’ uliofanyika katika shehia ya Mtoni kufuatia maombi ya wananchi hao kutaka kukutana na mkuu wa wilaya ili kumuelezea matatizo waliyonayo.

Wamesema eneo la Mtoni Kijundu kutokana na ukuaji wake limekosa huduma muhimu za kijamii ikiwemo miundombinu mizuri ya barabara,maji safi na salama,kituo cha afya na skuli hatua ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao.

“Kutokana na mazingira ya huu mji wetu tunaomba tupatiwe hizi huduma muhimu maana kipindi cha masika tunakosa mawasiliano njia zote zinajaa maji huku hatutoki sababu mtaa huu umezungukwa na mito,” walisema wananchi hao.

Aidha wananchi hao wamemuelezea mkuu wa wilaya kusikitishwa kwao na vijana watoto wengi wa Mtoni Kijundu kukosa elimu ya dini na dunia kutokana na watoto hao kujishughulisha na mifugo ya mbuzi na ng’ombe wanayopewa na baadhi ya wazee.

“Watoto wetu hawasomi chuoni hawasomi skuli kutwa wanajishughulisha na uchungaji wa wanyama, kuna baadhi ya wazazi huwapa mifugo watoto wakachunge hatua ambayo inawakosesha kupata elimu,” walisema.

Akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Petter Kunambi, aliwahakikishia kuwa serikali itachukua juhudi za makusudi kuhakikisha inazipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazowakabili.

“Kwa kweli tumeona wenyewe baadhi ya matatizo yaliyopo katika eneo hili ikiwemo barabara maana hata mimi nimefika huku kwa tabu kutokana na uchakavu wa barabara mnayotumia,” alisema Suzan.