NA MWINYIMVUA NZUKWI, DODOMA

JAMII imehimizwa kushiriki michezo kama moia ya njia za kujikinga na maradhi  hasa yasiyoambukizika.

Akizungumza na wanamichezo katika tamasha la michezo kuadhimisha miaka 20 ya Mfuko wa taifa wa bima ya Afya (NHIF) kwa niaba ya mkuu wa mkoa Dodoma, Mkuu wa Wilaya Jabir Shekimweri  alieleza kuwa kushiriki michezo pia husaidia kupunguza gharama za matibabu.

Aidha aliwapongeza wanamichezo walioshiriki tamasha hilo kutoka taasisi mbali mbali wakiwemo wanahabari na kueleza kuwa ushiriki wa michezo pia huongeza ufanisi kazini.

“Ningewaomba waajiri na wafanyakazi kulipa umuhimu swala la mazoezi na michezo katika maeneo ya kazi kwani no njia sahihi ya kujikinga dhidi ya maradhi,” alieleza Shekimweri.

Awali mkurugenzi mkuu wa NHIF, Benard Kongwa alieleza kuwa tamasha hilo ni mwendelezo wa shughuli mbali mbali kuelekea katika kilelel cha maahimisho hayo mwezi ujao.

“Kwa muda sasa tumekuwa na mikutano na wadau mbalimbali lakini pia tuliona umuhimu wa kufanya bonanza hili ili kuamsha ari ya kufanya mazoezi kujikinga na maradhi, ” alieleza Kongwa.

Katika tamasha hilo, lilishirikisha michezo mbali mbali ikiwemo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba ambapo mbali ya michezo, chanjo ya kinga dhidi ya uviko 19 ilitolewa.