RIPOTI ya idadi ya watu ya mwaka 2000 huko nchini Brazil ilionyesha kwamba familia milioni 11.2 kati ya familia milioni 44.7 zinaongozwa na wanawake. Nchini Nikaragua 25% ya watoto huishi na mama zao pekee.

Mnamo mwaka 1990 huko nchini Costa Rica takwimu zilionyesha kwamba idadi ya watoto wasiotambuliwa kisheria na baba zao iliongezeka kutoka 21.1% hadi 30.4%.

Takwimu hizi zinaonyesha ni jinsi gani akina baba tunavyofeli katika suala zima la malezi ya watoto wetu huku majukumu mengi katika muktadha huu tukiwaachia akina mama pekee.

Mtafiti maarufu wa malezi nchini Poland, Jozef Augustyn aliwahi kueleza kuwa “Baba wengi hufikiri kuwa wao ni wazazi bora kwa sababu wanachuma pesa kwa ajili ya familia”.

Lakini hilo ni mojawapo tu ya majukumu ya baba. Ukweli ni kwamba watoto hawamthamini baba kulingana na kiasi cha pesa anazochuma au thamani ya zawadi anazowapatia, badala yake watoto hutaka upendo, wakati na uangalifu kutoka kwa baba na wala si zawadi. Hayo ndiyo mambo muhimu kwao.

Ushiriki wa baba katika malezi huleta usawa. Malezi ya watoto huhitaji usawa na hayahitaji kuegemea upande mmoja. Kimsingi, ni vyema tukatambua kwamba jukumu la malezi kwa watoto ni la wazazi wote wawili, wenye utu na maoni tofauti juu yao, wenye uwezo tofauti, udhaifu usiofanana na mitazamo tofauti. Wazazi wa namna hii huwafanya watoto wawe na uchaguzi wa njia sahihi zitakazowakuza na kuwaendeleza.

Malezi ya baba huwafanya watoto wawe na uelewa kuhusu wanaume. Msingi wa awali kabisa ambao mtoto hujengewa katika kuwatambua wanaume ni watu gani, wana tabia zipi, wanaonekanaje ni kupitia ushiriki wa baba kwenye malezi ambae kwao humuona kama mfano wa kuigwa.

Kupitia baba mtoto hupata uelewa juu ya kulinda, kutoa, uhuru, kufanya kazi kwa bidii na ukomo wa mamlaka, hupata fursa ya kujifunza namna ya kuwa Baba mwema kwa mtoto wa kike ni funzo la namna ya kuchagua mwanaume sahihi pindi awapo mtu mzima.

Uhusika wa baba katika malezi husaidia kujenga upendo kwa mtoto. Upendo na ukaribu uliopo kati ya mtoto na mama huwa ni wa moja kwa moja tangu mtoto anapozaliwa. Tofauti na upande wa baba ambapo upendo huu unahitaji kupaliliwa na baba mwenyewe kwa kuonyesha ushirikiano na jitihada katika malezi. Kwa kuwa upendo huu hujengwa basi mtoto anapompenda baba yake inakua rahisi kumuamini.

Humjengea mtoto uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali. Mara nyingi mtoto mwenye mahusiano mabaya na baba yake huwa na msongo wa mawazo na kuhisi upweke.

Japo mama yupo lakini aonapo wenzie wazazi wote wanahusika na malezi huona kwamba yeye si mkamilifu. Na mara nyingi anaweza kuiga tabia zisizofaa mitaani mfano madawa ya kulevya, pombe na vilevi mbalimbali ili kuepukana na msongo huo wa mawazo.

Kama tunakubaliana na ukweli kwamba mtoto hawezi kuzaliwa bila ya baba na mama basi tukubaliane pia kuwa mtoto hawezi kukamilika bila baba na mama. Nafasi ya baba katika malezi haiwezi kulinganishwa na kitu chochote kile. Baba simama, shiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya mtoto.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org