NA MWAJUMA JUMA

WIZARA wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema ligi ya soka la  Ufukweni inatarajiwa kuanza kuchezwa  msimu wa mwaka 2021/2022.

Akijibu suali la mwakilishi Hassan Hamad Omar (Jimbo la Kojani) kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Leila Mohammed Mussa, alisema utaratibu wa kuanza ligi hiyo tayari umeanza.

“ Mheshimiwa Spika, Kamati ya Mpira wa Ufukweni  imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya ZFF na utaratibu wa kuanzisha ligi ya mashindano hayo umeanza na utaanza kwa msimu wa mwaka 2021/2022”, alisema.

Hata hivyo alisema kwamba kwa sasa hakuna ligi rasmi ya soka la Ufukweni, ila timu hizo zinakuwa zinashiriki mashindano mbali mbali na  hupata mialiko ya kushiriki mashindano Tanzania Bara na Kenya.

Aidha alisema hivi sasa Zanzibar kuna jumla ya timu nane  za mchezo huo  ambazo zimesajiliwa na Mrajisi wa vyama vya michezo na klabu.

Alizitaja timu hizo kuwa ni Lavista, Bububu Star na Green River (za Bububu); Alnnur, Zanzibar Swimming, Malindi Star (za Malindi) na Mahonda ya Mahonda na Blue sea (Jang’ombe).