NA MAKAME MASOUD,MUM

OFISA Mdhamini Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii Wazee, Wanawake na Watoto, Yakoub Mohamed Shoka, amewakaribisha madaktari bingwa kutoka China katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani.

Akizugumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege waa Karume, Shoka alisema timu ya madaktari tisa kutoka China watakuwepo katika hospitali hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja pamoja na za Chake Chake na Micheweni.

“Madaktari hawa watafanya kazi zaidi katika hospitali ya Aballah Mzee iliyopo mkoani lakini pia watakwenda hospitali ya Chake Chake na Micheweni,” alisema.

Aliwataka  madaktari hao kutokuwa na hofu na wajihisi kama  wapo nyumbani.

Alifafanua kuwa upatikanaji wa madaktari hao utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa matibabu bora katika kesi za mifupa na ajali hususan kwa wakaazi wa kisiwa cha Pemba.

Aliishukuru serikali ya China kwa kuleta madaktari kila mwaka nchini tokea Zanzibar ilipopata uhuru mwaka 1964.

Kiongozi wa madaktari hao, Dk. Li, alisema watafanya kazi kwa umakini na bidii kubwa ili kuboresha afya za wananchi.“Tutafanya kazi kwa bidii na umakini mkubwa katika kipindi chote tutakachokuwepo hapa,” alisema.