NA ALI KINASA, MUZNAT HAJI (SCCM)

MADEREVA na Makonda wa gari za abiria za Wilaya ya Kati wameipongeza serikali kwa uwamuzi wake wa kuhamisha kituo cha gari hizo kutoka Mwembeladu hadi Kijangwani, hali iliyosaidia kuondosha usumbufu.

Waliyasema hayo, jana walipozungumza na Zanzibar Leo, hapo kituo kipya cha Kijangwani Wilaya ya Mjini Unguja.

Mmoja wa madereva hao Ramadhan Ali, alisema uwepo wa kituo cha gari za abiria eneo la Kijangwani umewarahishia upatikanaji wa abiria kwa wingi, ukilinganisha na kituo cha awali, kutokana na eneo hilo kuwa katikati ya mji.

“Abiria wanakuja kwa wingi kwa sababu hapa nahisi ni eneo lililo senta ya mji, kwani kila abiria kutoka pande zote unampata kwa urahisi” alibainisha.

Aidha, Ramadhan alisema eneo la kituo cha Kijangwani ni kubwa ukilinganisha na kituo cha Mwembeladu, hatua ambayo inatoa wigo kwa gari hizo kupata nafasi ya kutosha ya kuegesha kwa ajili ya kusubiria abiria bila usumbufu wowote.

Akizungumzia mtazamo wake, Khalid Idrissa, alisema anaishukuru serikali kwa kufanya uhamisho wa kituo cha Mwembeladu hadi Kijangwani, kwani utaratibu wake umekua ni rafiki.

Aliongezea kwa upande wa changamoto inayowakabili, ni kuhusu kituo cha kukalia abiria kutawaliwa na jua na kupelekea shida nyakati za mchana kusubiria daladala katika kituo hicho.

Hata hivyo, aliiomba serikali kuengeza sehemu za makaazi ya abiria ili wapate kukitumia  wakisubiri gari wazitakazo ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa ni kidogo, hali ambayo inaleta usumbufu.