NA AMINA AHMED
MAHAKAMA ya Mkoa ‘B’ Chake Chake, imeanza kusikiliza mashahidi wawili kwa upande wa walalamikaji dhidi ya kesi namba 7/21, inayomkabili Rashid Buda Abdalla (40) mkaazi wa Madungu Chake Chake Pemba anaekabiliwa na makosa mawili tofauti.
Mashahidi hao wamesikilizwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoe Nyengo na chini ya mwendesha mashtaka wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DDP, Ali Amour Makame.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka DPP Ali Amour Makame, mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ambayo ni kosa la kutorosha msichana na kosa la shambulio la aibu.
Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa mnamo siku ya Machi 2 mwaka huu majira ya saa mbili za asubuhi mshitakiwa huyo alimtorosha msichana wa miaka 9 huko Madungu Chake Chake bila halali na bila ridhaa ya walezi wake kutoka nyumbani kwao na kwenda nae katika banda la Ng’ombe hapo hapo Madungu jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hata hivyo mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa kosa la pili kwa mshitakiwa huyo kuwa ni shambulio la aibu ambapo alidai kuwa kwa njia ya aibu alimvua chupi na kumshika sehemu zake za siri za mbele msichana huyo jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kutorosha msichana ni kosa kwamujibu wa kifungu cha 113 (1) (a) sheria ya adhabu sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya zanzibar.
Shambulio la aibu ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 114 (1) sheria ya adhabu sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Aidha baada ya kusikilizwa kwa mashahidi hao upande wa walalamikaji Hakimu wa Mahakama hiyo Luciano Makoe Nyengo alipanga tarehe nyengine ya kuendelea kusikiliza mashahidi wengine ambayo ni siku ya tarehe 28/10/ 2021 kwa ajili ya kuendeleza ushahidi dhidi ya tuhuma hizo kwa kusikiliza mashahidi wa upande wa mshitakiwa .
Wakati huo huo Mahakama hiyo itaendelea kusikiliza zaidi ya kesi tano mfululizo dhidi ya makosa ya udhalilishaji ambapo kwa nyakati tofauti mahakama hiyo ilisema itaendelea kusikiliza tena kesi namba , 06/2020 inayomkabili Maulid Said Moh’d Mkaazi wa Michenzani anaekabiliwa na tuhuma ya shambulio la aibu kwa mtoto wakiume siku ya tarehe 28/10 /2021.