NA MARYAM HASSAN

WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale kupitia Mamlaka ya Uhifadhi na Uendeshaj Mji Mkongwe imekabidhi majengo 20 kwa ajili ya uwekezaji katika awamu ya kwanza ya mpango wa ukodishwaji wa majengo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Wizara hiyo Leila Mohammed Mussa, wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Unguja.

Alisema uwekezaji huo unategemea kufikia takriban shilingi bilioni sita ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kutengeneza majengo yaliyokuwa hatarishi ndani ya Mji Mkongwe.

Alisema lengo ni kuyanusuru na kuyarudisha katika haiba ya mji na kutengeneza miundombinu ya barabara, majisafi na maji taka na umeme ndani ya Mji mkongwe.

Waziri Leila alisema, maombi hayo yalianza tokea Juni 21, mwaka huu hadi Julai 9 mwaka huu ambapo maombi ya awamu ya pili yalitangazwa Septemba 20 mwaka huu hadi Otoba 15 mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu masharti ya maombi kwa wawekezaji hao, alisema lazima muombaji apendekeze atalipa kiasi gani kwa serikali kwa ajili ya jengo au eneo ambalo anataka kuwekeza.

Masharti mengine ni kuainisha aina na lengo la uwekezaji wake kwa jengo au eneo husika.

Muombaji aeleze jinsi gani kajipanga kulitengeneza jengo hilo na uzowefu wake katika kuendesha shughuli anayotaka kuiwekeza Mji Mkongwe.

Pia alisema muombaji lazima awe tayari wakati wa ujenzi kufata masharti ya ujenzi katika eneo la urithi wa Dunia chini ya usimamizi wa wataalam kutoka Mamalaka ya Uhifadhi na Uendeshaji wa Mji Mkongwe.

Sambamba na hayo alifafanua kuwa mwekezaji huyo atatozwa kiasi cha kodi kulingana na gharama zitakazotumika katika ujenzi wa jengo au eneo la uwekezaji.

Pia alisisistiza kuwa majengo ambayo yameshatolewa yasiombwe tena na badala yake kufuata maelekezo kwa majengo mapya.

Akitaja majengo ambayo yamekabidhiwwa kwa wawekezaji kwa awamu ya mwanzo Waziri Leila alisema jengo namba 27, 28, 18C/D/E, SHIH, Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mjini, yote yapo Shangani.

Jengo 580(IPA), 566 Shangani, Hamamni Bath Kajificheni, 2010 Kajificheni, 712/17 Malindi, 40 Shangani, 1195 Malindi 1188/90 Malindi, 65 Shangani, 66 Shangani,794 Kiponda.

Majengo mengine ni namba 83 A (Tume ya Ukimwi) Shangani, 2361/62 (Bekar ya Vuga) kiwanja cha nyumba namba 31 (Jumuiya ya wazazi CCM) 1,491 Kiponda na 2,206 Kajificheni.

Aidha aliwataka wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya kihistoria kwa wananchi wote wanaoishi ndani na nje ya nchi.