Ni utekelezaji la kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalumu la kimkakati

Na Rajab Mkasaba

UJENZI wa jengo jipya la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Pemba ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utendaji na utoaji huduma kwa wananchi.

Majengo ya kisasa yaliyojengwa sio tu kwamba yana mchango mkubwa katika mazingira ya kufanyia kazi bali pia yanaongeza taswira ya mji pamoja na kuufanya mji Chake Chake Pemba, uwe wa kupendeza.

Ujenzi wa ofisi za kisasa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalum la kimkakati la uwekezaji sambamba na kuhakikisha kwamba huduma na mahitaji muhimu kwa wananchi na wawekezaji yanayopatikana Unguja pia, yapatikane kisiwani Pemba.

Jengo hilo ambalo litakuwa na ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato (ZRB) ndani yake litasaidia katika kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Ni wazi kwamba, kazi ya Ujenzi wa jengo hilo ni matokeo ya mikakati mizuri ya Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa lengo la  kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Serikali zote mbili zina jukumu la kuhakikisha kwamba inaziwekea mazingira mazuri Taasisi hizo kwa kuwawekea vitendea kazi vya kisasa na watendaji wazalendo, wachapakazi, waadilifu na wenye kuchukia rushwa na vitendo vyote vya ubadhirifu wa mali ya umma .

Ujenzi wa jengo hili la ZRB kisiwani pemba ni wazo la kimaendeleo kwa  matumizi bora ya ardhi na utekelezaji kwa vitendo wa Mipango Miji iliyopitishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ujuzi, maarifa  na uzoefu uliopatikana katika ujenzi wa jengo hili  utakuwa ndio dira ya kutekeleza dhamira  ya kujenga majengo mapya ya   taasisi mbali mbali za Serikali Unguja na Pemba.

Katika kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi,  Serikali  itaendelea kujenga majengo ya kisasa yanayopendeza na  kuvutia na kuweka vifaa vya kufanyia kazi  vinayovyoendana na mabadiliko, pamoja na  mahitaji ya wakati huu.

Azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi yameelezwa bayana katika Mkakati wa Mabadiliko katika Utumishi wa Umma, ulioandaliwa mwaka 2010 kupitia Eneo la Pili la Kimkakati inaloazimia katika  kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi ya watumishi wa umma.

Kwa hakika mazingira ya jengo hili ni mazuri na yanavutia hivyo, wafanyakazi watakaofanya kazi kwenye jengo hili watayatumia mazingira haya bora  kwa kuongeza kasi, ari na mapenzi katika utendaji wa  kazi zao kwa lengo la  kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.

Tayari haiba ya mji wa Chake Chake katika eneo la Gombani inaendelea kubadilika kila uchao kutokana na kuongezeka kwa majengo yanayovutia likiwemo jengo hili.

Lakini ni lazima wananchi wakajidhatiti na kuendelea kushirikiana na Serikali yao ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi katika kuifanya kazi hii ya kuiimarisha miji kwa bidii kubwa huku wakitilia maanani msemo usemao “ Roma haikujengwa kwa siku moja”. 

Jengo hili sehemu lilipojengwa ni pahala pazuri na jinsi lilivyo linamvutia kila mtu wakiwemo wageni wetu wanaokuja kuitembelea Pemba kwa shughuli mbalimbali na hata Watalii wataweza kuvutiwa na jengo hili. Jengo hili lina uzuri wa pekee kama linavyoonekana.

Kwa hakika, inapendeza kuona kwamba  katika eneo hili la Gombani tayari yapo majengo ya Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye hadhi ya kileo na yanayovutia.

Hatua hii ya kujenga jengo  hilo la kisasa kando ya mji kutasaidia sana katika kupunguza msongamano wa gari  katika mji wa Chake Chake, jambo ambalo linatoa faraja na afuweni kwa wafanyabiashara na wananchi wanaoendesha shughuli zao nyengine  za kiuchumi na kijamii katika mji huo.

Ni vyema ikazingatia hekima ya wazee kwamba kitunze kidumu, haiba ya jengo hili na umadhubuti wake utategemea juhudi za wafanyakazi watakaofanya kazi dnani ya jengo hilo katika jukumu zima la kulitunza.

Suala la matunzo ya majengo na vifaa vya ofisi ndani ya Wizara za Serikali ni jambo la lazima kwa kila Wizara husika kwani kama inavyotambulika kwamba Wizara ina wajibu wa  kuhakikisha kwamba  inatenga fedha kila baada ya muda kwa ajili ya matengenezo ya jengo yao ya ofisi kwani wahenga walisema “ Usipoziba ufa utajenga ukuta”.

Kila kiongozi wa Serikali anapaswa kufahamu mipango mikuu ya serikali na ahadi zinazotolewa na viongozi na kuandaa mikakakti ya utekelezaji kwani Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwka 2020-2025 imeelekeza kwamba ukusanyaji wa mapato wa Zanzibar uongezeke kutoka Bilioni 800 hadi kufikia Trilioni 1.5 katika kipindi cha miaka mitano.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuamua kufanya kazi pamoja kati ya TRA na ZRB katika jengo hilo jipya ni za msingi na zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kazi sanjari na kuiwarahisishia wananchi katika kupata huduma zao stahiki.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inataendeleleo kufanya kazi na ZRB pamoja na TRA katika kuhakikisha kwamba kila mwananchi anaestahiki kulipa kodi anafanya hivyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi mara baada ya kulizindua jengo hilo la ZRB kiwasni Pemba katika hotuba yaker alisema kwamba yeye si muumini wa utozaji wa kodi kubwa.

Katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 marekebisho makubwa ya usimamizi ya kodi yamefanyika kwa lengo la kushajiisha kulipa kodi kwa hiyari na kumpa  unafuu kubwa mfanyabiashara.

Rais Dk. Mwinyi alisema kazi kubwa imefanywa na Serikali ya awamu ya Saba katika kuimarisha mazingira mazuri ya kufanyiakazi  kisiwani Pemba ambapo yapo majengo mazuri ya Serikali yalijengwa katika eneo hilo la Gombani jirani na jengo hilo jipya la ZRB, ambapo pia kuna jengo la  Mfumo wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)  alilolizindua mnamo Januari 05, 2021 pamoja na majengo mengine mengi.

“Serikali ya awamu ya saba, ilianya kazi kubwa kwa kuimarisha mazingira mazuri ya kufanyia kazi hapa kama yale tulio yaona na lile la Ofisi za ZSSF na laeo hii tunafunguwa hili la ZRB,” alisema Rais Dk. Mwinyi.

“Kwa ujumla kila Wizara inayo ofisi ya kisasa kisiwani  Pemba ,majengo hayo yaliojengwa sio tu kuwa yana mchango  mkubwa katika kuimarisha ufanyaji kazi bali pia yanaimarisha taswira ya mji na kuufanya   uwe wa kupendeza”.

Rais Dk. Mwinyi alifahamisha ujenzi wa Ofisi za kisasa ni hatuwa muhimu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalumu la kimkakati la uwekezaji na Serikali itahakikisha kwamba huduma na mahitaji  muhimu kwa wananchi na wawekezaji yanayopatikana Unguja vile vile, yanapatikana Pemba.

“Bado tunadhamira ile ile ya kunakifanya Kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalumu la kimkakati la uwekezaji, sasa ujenzi wa ofisi kama hizi za kisasa ni hatuwa muhimu ya utekelezaji kwani tumedhamiria kuona mahitaji muhimu kwa wananchi na wawekezaji yanayopatikana Unguja na Pemba yanakuwepo,”alifahamisha  Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi katika hotuba yake hiyo za uzinduzi wa jengo hilo alisema kuwa ni kweli bidhaa zimepanda bei huko zinakonunuliwa kutokana na kuwepo kwa UVIKO  19, ambapo bei zimepanda kutokana na usafiri na kulepelekea bidhaa kutoka nje zipande bei.

Hata hivyo, Serikali imefanya juhudi za kupunguza kodi kwa bidhaa mbali mbali zinazotoka nje hivyo, wafanyabiashara wataona dhamira hiyo ya serikali na hwatopandisha bei ya bidhaa bila ya sababu.

Rais Dk. Mwinyi alitoa onyo kali kwa wale wanaotumia hali hiyo kwa kupandisha bei kama vile saruji kutoka Dar-es-Salaam ama Mtwara na kuzitaka taasisi husika kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaoongeza bei bidhaa.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wajenzi wa jengo hilo pamoja na wakandarasi, mafundi, vibarua na wale wote walioshiriki katika ujenzi huo ikiwemo Kampuni ya ujenzi na wale  waliotoa tenda ambao wamefanya vizuri na thamani ya fedha imeonekana katika jengo hilo.

Jengo  hilo linachochea utulivu wa kufanyia kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi ambapo kutokana na miundombinu yake litakuwa na usalama wa kutosha na ulinzi pamoja na utunzaji bora wa kumbukumbu wa nyaraka kutokana na mfumo uliojengwa wa tehama katika jengo hilo.

Pia, litakuwa na kitengo cha dharura, na kuwa na huduma za kuaminika hasa huduma za umeme ambapo litakuwa na umeme muda wote hata pale huduma hiyo ikikosekana.

Jengo hilo jipya lina ghorofa nne, ghala, na sehemu nyenginezo, ambapo kuanzia ghorofa ya kwanza hadi ya nne kuna vyumba kwa ajili ya wafanyakazi mbali mbali, pamoja na kuwepo kumbi mbali mbali na sehemu nyengine muhimu ndani ya jengo hilo.

Mkataba wa ujenzi wa jengo hilo ulitiwa saini mwezi Disemba 2019 kati ya ZRB na Mkandarasi ‘Advent Construction Limited’ kutoka Dar-es-Salaam na kukamilika rasmi mwezi Mei mwaka 2021 kwa gharama za Shilingi Bilioni 10.6.

Lengo la kujenga ofisi mpya na nzuri ni kwa ajili ya kuwapatia wafanyakazi maeneo mazuri ya kufanya kazi na kuwaweka katika mazingira bora ya kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi hatua ambayo itawapelekea wafanyakazi kuridhika kwani iwapo wafanyakazi wataridhika ndipo wataweza kufanya kazi ipasavyo.