NA MWANDISHI WETU

MAKARANI na wasimamizi wa sensa ya majaribio  ya watu na makaazi, wametakiwa kuthamini na kuenzi wajibu waliopewa na kuonesha uzalendo kwa nchi wakati wa kutekeleza majukumu ya kukusanya taarifa za zoezi hilo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alipokuwa akifunga mafunzo hayo huko Tunguu, wilaya ya Kati Unguja jana.

Alisema, lengo la Sensa ya Majaribio ni kupima utayari wa kufanya sensa kuu, hivyo, makarani na wasimamizi wana dhima kubwa ya kuhakikisha sensa ya 2022 inafanikiwa na kufikia malengo ya serikali yaliowekwa.

“Kupitia madodoso na muundo wa maswali, makadirio ya muda utakaohitajika kufanya sensa, kupima ukamilifu wa matumizi ya teknolojia itakayotumika, ni miongoni mwa mafunzo hayo.

“Tunachokiamini sasa mmeshawiva na mpo tayari kwa jukumu hilo kubwa la kitaifa kwani mafanikio ya sensa ya majaribio yanategemea ufanisi wa kazi yenu,” alieleza Haroun.

Mapema, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mayasa Mahfoudh Mwinyi, alisema, mafunzo hayo ya siku 16 yamewashirikisha washiriki kutoka kwenye maeneo yaliyochaguliwa  kufanyiwa  majaribio ya sensa.