NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania na Sekta binafsi zimesaini hati ya makubaliano ya kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo jana, Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Gerald Kusaya, alisema utiaji wa saini huo, utawezesha kuanza utekelezaji wa makubaliano kama ilivyoainishwa kwenye kanuni juu ya ushirikiano wa pande zote mbili.

Alisema mkataba huo utaanza na kampuni 32 na vyama viwili vinavyohusika na uzalishaji na uingizaji wa kemikali nchini vya TPMA na TAPI na wadau wanaojihusisha na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Aidha aliwashukuru wadau mbali mbali kwa kuonesha utayari wa kuiunga mkono serikali kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kitaifa na kimataifa.

“Tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwa na vikao vya pamoja, kupitia na kuimarisha kanuni ambazo kwa ujumla zinaainisha namna ya ushirikiano utakavyotekelezwa na kuimarisha mifumo ya kupeana taarifa,” alisema.

Aliongeza kwamba ili kuendelea kukabiliana na changamoto ya uchepushaji wa kemikali hizo, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na mamlaka ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Dawa Tiba, Bohari Kuu ya Dawa, Baraza la Famasi nchini na sekta binafsi inatekeleza mradi wa pamoja chini ya uratibu wa bodi ya kimataifa ya kudhibiti dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa mradi huo umelenga kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana kati ya mamlaka na sekta binafsi ili kuimarisha na kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fiderice Mafumiko, alisema serikali imetunga sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ili kudhibiti dawa za kulevya na uchepushaji wa kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.

Kwa upande wake Makamu   Mwenyekiti wa TAPI, Churchill Katazwa, aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kufikia makubaliano yatakayosaidia kuokoa nguvu kazi ya taifa.

Alisema jukumu hilo litawasaidia waagizaji na wasambazaji kusimamiana wenyewe na kupeana elimu ili dawa zitumike kwa matumizi yaliyopangwa na serikali.