NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema kuanzia mwezi Aprili hadi Agosti mwaka huu, imekamata zaidi ya kilo 900 za dawa za kulevya aina ya ‘heroin’ na ‘methamphetamine’.

Kamishna wa Divisheni ya Kinga na Tiba wa Mamlaka hiyo, Dk. Peter Mfisi, alieleza hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipozungumza na waandishi wa habari.

Dk. Mfisi alisema mamlaka hiyo, ipo kwenye mazungumzo na wataalamu wa wizara ya Elimu ya katika kuangalia namna ya kuingiza katika mtaala wa elimu ya msingi somo la dawa za kulevya ili kupunguza athari za matumizi za dawa hizo hasa kwa vijana.

Alisema lengo la kuingiza mtaala huo, ni kusaidia jamii ufahamu wa madhara ya dawa za kulevya wakiwa katika elimu ya msingi kwa vile asilimia 99 ya watanzania wanasoma skuli ya msingi.

Akizungumza jana jijini hapa, Kamishna wa Divisheni ya Kinga na Tiba wa Mamlaka hiyo, Dk. Mfisi alisema kwa kipindi kifupi wamekamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya, jambo ambalo haijawahi kutokea kukamata kiasi hicho huko nyuma.

Alisema kwa mwezi Aprili mwaka huu wamekamata kilo zaidi ya 800 za ‘heroine’ na ‘methamphetamine’.

Aidha alisisitiza kuwa sio kila dawa ya kulevya inayoingia nchini inatumika Tanzania, bali sehemu kubwa inatoka nje ya nchi na kupelekwa mahali pengine.

Alisema zinasafirishwa kuanzia Somalia, Kenya, Tanzania, Msumbiji, zinakwenda hadi Afrika Kusini ambapo zikifika huko husafirishwa kupelekwa nchi nyingine, uingiaji umekuwa rahisi kwa sababu ya maji.

“Kutoka Tanga hadi Mtwara kuna bandari bubu zaidi ya 400 ambazo mtu anaweza kuingia bila kujulikana, lakini sisi tunafanya juhudi kufanya doria kubwa kwenye maji kabla hawajafika kwenye bandari bubu”, alisema.

Alisema kuna vituo 11 vya kurekebisha tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya ambapo hadi mwezi Juni mwaka huu walikuwa na watumiaji waliosajiliwa katika vituo hivyo 10,565.