LONDON, England
MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema, alihisi ‘mwenye hatia’ baada ya timu yake kushindwa kuonesha kiwango katika sare ya bila ya kutofungana na Southampton kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England uliochezwa uwanja wa Etihad.
Guardiola hapo awali alikuwa amekataa kuomba radhi kwa kuwataka mashabiki wa ManCity kuhudhuria mchezo huo baada ya ushindi wa magoli 6-3 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig.
Kikosi chake kilifanikiwa kupiga shuti moja tu kwa lango katika mchezo huo ulionekana mgumu kwa mabingwa hao watetezi wa England.
“Siku zote wakati mchezo usio mzuri najisikia vibaya”, alisema, Guardiola.
“[Mashabiki] wanakuja kuona onyesho bora, kuona mchezo. Wakati haifanyiki ninajisikia hatia kidogo kwa sababu hatukucheza vizuri.
Mahudhurio rasmi kwenye Uwanja wa Etihad yalikuwa ya mashaibiki 52,698, makubwa zaidi ya ManCity msimu huu hadi sasa na zaidi kuliko umati wa mashabiki 38,062 dhidi ya Leipzig kati kati ya wiki, lakini, msaada huo mkubwa wa nyumbani haukuwahamasisha mabingwa hao watetezi mbele ya ‘Watakatifu’.
Guardiola alisisitiza baadaye kwamba maoni yake baada ya ushindi wa kundi ‘A’ yalitafsiriwa vibaya.
“Sikusema chochote kibaya baada ya Leipzig,” alisema. “Nilisema tulikuwa na mchezo mgumu dhidi ya Southampton na tungehitaji msaada kutoka kwa mashabiki.
“Sikuwahi kulalamika juu ya mashabki wangapi wanaokuja au hawaji. Sijawahi kufikiria hili maishani mwangu. Sijui ni kwanini watu wananiuliza swali hili. Nashukuru hata kama watu 85 au 100 watakuja.”
ManCity walikuwa masikini bila ya umiliki wa mchezo na walikosa cheche zao za kawaida za kushambulia dhidi ya kikosi cha Ralph Hasenhuttl, na juhudi zao tu kwenye lango zilipatikana katika dakika ya 90.
“Hatukuwa wazuri katika ujenzi wetu, tulipoteza mipira rahisi katika mchakato wetu kwa sababu hatukuwa wajanja na wazembe kidogo”, aliongeza, Guardiola.
“Ndio maana lazima nipongeze Southampton. Tunasonga mbele”.