NA ASIA MWALIM

BARAZA la Manispaa Mjini limesema limekusudia kufanya tathmini ya kuona namna ya kuanza ujenzi wa mtaro wa eneo la Chumbuni ili kuondoa tatizo la kuingiliwa na maji katika kipindi cha muda mrefu.

Alisema tathmini hiyo itafanikisha kupata gharama za ujenzi wa mtaro huo na kuweza kupanga mikakati ya kuanza shughuli za ujenzi katika kipindi kifupi kinachokuja.

Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Mjini, Ali Haji Haji, alisema hayo alipokuwa akizungumza na Zanzibar leo Ofisini kwake Malindi Zanzibar.

Alisema kupatikana kwa taarifa ya tahtmini hiyo kutawakutanisha viongozi hao kujadili kwa kina namna ya kuanza ujenzi huo ili kuondoa kero iliyowakabili wananchi kwa muda mrefu.

Alifahamisha kuwa baraza hilo kupitia viongozi wake litaedelea kufanya upembuzi yakinifu ili kuona namna ya kuondoa tatizo hilo sambamba na kuimarisha maendeleo ya nchi kiujumla.

Alieleza kuwa kutokana na kuguswa kwa kiasi kikubwa baraza hilo linafanya juhudi za kuondoa matatizo yanayowakabili wananchi wake hivyo linachukua jitihada za makusudi kuleta maendeleo.

Alisema ushiriki wao katika masuala ya maendeleo ni jambo muhimu linalohitajika kupewa kipaumbele na kila mtu ili kusaidia kufikia azma ya serikali katika mikakati na mipango ya maendeleo kwa ngazi za shehia hadi taifa.

“Tunasubiri tathmini ya watendaji wetu kuniletea tuweze kukaa pamoja na kuendesha vikao vyetu kwa haraka kutokana na maeneo hayo kutoridhisha” alisema.